Mwanasheria  Mkuu wa serikali,Hamza Johari  akifungua mafunzo  kwa mawakili wa serikali yanayofanyika kwa muda wa siku tatu jijini Arusha .
Mwanasheria  Mkuu wa serikali,Hamza Johari  akifungua mafunzo  kwa mawakili wa serikali yanayofanyika kwa muda wa siku tatu jijini Arusha 
……..
Na Happy Lazaro, Arusha 
MAWAKILI  wa serikali wametakiwa kuwa vinara wa mabadiliko na si wasimamizi wa kawaida wa sera na sheria, ili kuhakikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inatekelezwa kwa ufanisi na kuifikisha Tanzania katika uchumi wa kisasa unaoshindana kimataifa.
Hayo yamesemwa  leo jijini Arusha na Mwanasheria  Mkuu wa serikali,Hamza Johari wakati akifungua mafunzo kwa mawakili wa serikali yanayofanyika kwa muda wa siku tatu jijini Arusha.
Amesema kuwa,mafunzo kwa Mawakili wa Serikali  yanalenga kuwajengea uwezo wa kitaaluma ili waweze kuchangia kikamilifu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hususan katika maeneo ya mikataba, uwekezaji na uoanishaji wa sheria na mahitaji ya maendeleo ya Taifa.
Aidha amesema mafunzo ya awali yalijikita katika masuala ya ufundi wa sheria, usimamizi wa mikataba pamoja na mbinu mbalimbali za kuongeza ufanisi wa utendaji wa Mawakili wa Serikali.
“Mada zilizopangwa katika mafunzo hayo zimeandaliwa kwa kuzingatia mahitaji halisi ya wakati, huku zikilenga kuwajengea washiriki uwezo wa kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa majukumu yao.”amesema Johari.
Aidha, amebainisha kuwa kwa upande wa sekta ya sheria bado kuna jukumu kubwa la kuhakikisha sheria za nchi zinaoanishwa na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ili ziwezeshe utekelezaji wa sera na miradi ya maendeleo kwa ufanisi zaidi.
Amesisitiza pia umuhimu wa Mawakili wa Serikali kubadili mtazamo wa utendaji na kuwa wataalamu wanaoweza kushiriki kikamilifu katika majadiliano na utekelezaji wa mikataba na shughuli mbalimbali za maendeleo, sambamba na kutoa ushauri wa kisheria unaokwenda sambamba na mahitaji ya uchumi wa kisasa.
“Maandalizi ya mafunzo hayo yaliongozwa na maswali muhimu yanayolenga kutafakari nafasi ya Mawakili wa Serikali katika kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ili kupitia mada mbalimbali washiriki wapate majibu na kuongeza uelewa wao.”amesema Johari.
Ameongeza kuwa matarajio ya mafunzo hayo si kutoa majibu pekee kwa maswali yaliyoibuliwa, bali pia kuboresha maarifa, kuongeza uwezo wa kitaaluma na kuwawezesha Mawakili wa Serikali kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi katika kuharakisha maendeleo ya taifa.
Johari amesema lengo kuu la Dira ya Maendeleo 2050 ni kuleta mageuzi ya kiuchumi (economic transformation), huku akisisitiza kuwa serikali ndiyo daraja muhimu la kufanikisha safari hiyo kupitia sera, sheria, kanuni na miongozo inayoweka mazingira bora ya maendeleo.
Amesema wakati wa kuandaa mafunzo hayo waandaaji walijiuliza kama mafunzo hayo yatakuwa na mchango wa kweli katika utekelezaji wa dira hiyo. 
Amefafanua  kuwa walijiridhisha kwamba mada zilizopangwa zitawapa washiriki majibu ya maswali muhimu pamoja na kuongeza uelewa na maarifa yatakayowasaidia kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
“watendaji wa serikali hawapaswi kuwa viongozi wanaosubiri mabadiliko yatokee, bali wanapaswa kuwa mabingwa (champions) wa maendeleo watakaosukuma mbele utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.”amesema Johari.
Amebainisha kuwa utekelezaji wa dira hiyo unahitaji watendaji wenye maarifa ya kisasa yanayozingatia sheria, uchumi, biashara, teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), pamoja na uelewa wa mabadiliko ya mazingira ya kijiografia na kisiasa duniani (geopolitics), ili kufanya maamuzi yanayokwenda sambamba na kasi ya dunia.
“Mafunzo haya yanatoa nafasi ya kujadili namna bora ya kupata rasilimali za kifedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo, akibainisha kuwa takribani asilimia 70 ya fedha zinazohitajika kufanikisha Dira ya Maendeleo 2050 zinatarajiwa kutoka sekta binafsi.”amesema .
Aidha amewataka watendaji wa serikali kuimarisha matumizi ya ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati, akisema ushirikiano huo ni nguzo muhimu ya kukuza uchumi endelevu na kuhakikisha taifa linapata rasilimali za kutosha kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Naye Mkurugenzi wa Uratibu na Huduma za Ushauri, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,Wakili  Neema Ringo  amewataka Mawakili wa Serikali kuhakikisha sheria za nchi zinaendana na mahitaji ya sasa ili kuchangia kikamilifu utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, sambamba na kukabiliana na mabadiliko ya sayansi, teknolojia na mazingira ya kisheria yanayoendelea duniani.
Amesema kuwa utekelezaji wa Dira ya 2050 unahitaji mchango mkubwa wa wataalamu wa sheria, hususan katika kupitia, kurekebisha na kutunga sheria zitakazowezesha kufikiwa kwa malengo ya maendeleo ya Taifa.
“Wakati wa uandaaji wa Dira ya 2050, Serikali ilitoa maelekezo mahsusi kwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Tume ya Kurekebisha Sheria ya Tanzania kufanya mapitio ya sheria zilizopo ili kubaini zinazohitaji marekebisho, kufutwa au kutungwa upya kulingana na mwelekeo wa dira hiyo.”amesema Ringo.
Kwa upande wake Mwandishi Mkuu wa sheria ,Onorius Njole  amesema kuwa, kaulimbiu ya mafunzo inalenga kuwawezesha watendaji wa serikali kutumia taaluma ya sheria kwa ufanisi zaidi katika kusimamia shughuli za serikali na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Amesema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeendelea kutoa kipaumbele kwa ushiriki wa makundi maalum katika mafunzo hayo, hatua inayodhihirisha dhamira ya serikali ya kuhakikisha kila kundi linapata fursa sawa za kujiendeleza kitaaluma na kushiriki katika maamuzi muhimu.
Aidha, Njole amebainisha kuwa idadi ya washiriki kutoka makundi hayo imekuwa ikiongezeka kila mwaka, jambo linaloonyesha viongozi wa serikali wametambua umuhimu wa kuyawezesha makundi hayo na kuyaimarisha ili yatoe mchango mkubwa katika utumishi wa umma.