Wajumbe wa Chama Kikuu cha Ushirika wilayani Tunduru (TAMCU LTD) wakifuatilia mwendendo wa mnada wa nane na wa mwisho wa zao la ufuta kwa msimu 2025/2026 uliofanyika jana.

Kaimu Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika wilaya ya Tunduru(TAMCU LTD)Zainabu Sendema,akitoa taarifa ya kumalizika kwa minada ya ufuta kwa msimu wa kilimo 2025/2026 ambapo jumla ya kilo 2,147,796 zenye thamani ya Sh.bilioni 5,267,661.00 zimeuzwa.

…………

Na Muhidin Amri, Tunduru

CHAMA Kikuu cha Ushirika Wilaya ya Tunduru(TAMCU LTD)Mkoani Ruvuma, kimefanya mnada wa mwisho wa zao la ufuta kwa mwaka 2026 ambapo jumla ya kilo 64,295 zenye thamani ya Sh. 142,091,950.00 zimeuzwa katika mnada huo kwa bei ya Sh.2,210 kwa kilo moja.

Kaimu meneja wa Tamcu Zainabu Sendema alisema,mnada huo ulifanyika chini ya mfumo wa Soko la Bidhaa Tanzania (TMX)uliowezesha ushindani wa wazi kwa wanunuzi na kuwapa wakulima fursa ya kupata bei zenye tija ikilinganisha na mfumo wa soko huria.

Aidha alisema,katika msimu wa kilimo 2025/2026 Tamcu imefanya jumla ya minada minane iliyowezesha kukusanya na kuuza kilo 2,147,796 zilizoingiza Sh.5,267,575,661.00 huku bei ya chini ilikuwa Sh.2,210 bei wastani Sh.2,560 na bei ya juu Sh.2,452.

Sendema, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira rafiki ambayo yamewezesha Chama kikuu kuwasaidia wakulima kupata pembejeo kwa wakati zilizosaidia kupata soko la uhakika na kuongeza uzalishaji wa zao la ufuta,korosho na mazao mengine yanayouzwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani.

“Lakini tunamuomba aendelee kutusaidia pembejeo kwenye zao la ufuta lenye changamoto kubwa hasa wadudu wanaoshambulia maua,kama anavyofanya kwenye zao la korosho ili wakulima wazalishe kwa tija”alisema Sendema.

Amewataka wakulima,wasikate tamaa bali waendelee na kuzalisha kwa wingi mazao yote yaliyoingizwa kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani ikiwemo korosho na mbaazi ili waweze kunufaika na uwepo wa soko la uhakika.

Makamu Mwenyekiti wa Tamcu Kaisi Makolela alisema,bei nzuri na ushindani mkubwa wa wanunuzi umewanufaisha sana wakulima na ufuta wote ulioletwa kwenye vyama vya msingi vya ushirika(Amcos) uliuzwa,jambo lililoonyesha mahitaji ya zao hilo ni makubwa.

Makolela alisema,Chama kikuu kusimamia malipo yote ya wakulima na kusimamia masoko ya mazao ili wakulima waweze kunufaika kupitia shughuli zao la kilimo kama sehemu ya mkakati wa Chama katika kuhamasisha wakulima waongeze uzalishaji mashambani.

Akizungumza kwa niaba ya wakulima Msafiri Alaki, ameishukuru Serikali inavyosimamia sekta ya kilimo hususani soko la mazao tangu ilipoanzisha mfumo wa stakabadhi ghalani ambao una tija na manufaa makubwa kwa wakulima.

Alisema, kabla ya mfumo wa stakabadhi ghalani kuanza wakulima walikuwa na changamoto nyingi hasa bei ndogo ya mazao waliyozalisha kutoka kwa wafanyabiashara ambao walinunua mazao kwa bei ndogo isiyolingana na gharama za uzalishaji.

“Wakulima tumefarijika na tunaishukuru Serikali kusimamia soko na bei ya mazao yetu,hata hivyo tunaiomba isichoke kutafuta wanunuzi wengi zaidi ambao watakuja kununua kwa bei nzuri kwa kuwa mazao tunayozalisha kwa sasa yana thamani kubwa,Serikali ikae na wanunuzi na kupunguza mifumo ya kodi na ushuru ili wakulima wapate bei nzuri”alisema.