Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kwa kushirikiana na NMB imekabidhi kompyuta mpakato 10 zenye zaidi ya shilingi Milioni 18 kwa shule ya Sekondari Kwiro iliyopo katika Wilaya ya Ulanga Mkoani Morogoro ikiwa ni sehemu ya malengo iliyojiwekea katika sherehe ya kutimiza miaka 50 iliyofanyika mwaka 2025.

Kompyuta mpakato hizo zimekabidhiwa Julai 10, 2026 katika shule ya Sekondari ya wavulana Kwiro na kupokelewa na Mkuu wa Wilaya Mhe. Khamana Simba na kumkabidhi Afisa Elimu wa Wilaya Mwl. Kisiga ambaye alimkabidhi Mkuu wa shule Bw.John Kashamba.

Akipokea kompyuta mpakato hizo Mhe. Khamana Simba ametoa wito kwa walimu na wanafunzi wa shule ya Kwiro kuzitumia vizuri na kuzitunza ili zisaidie kuleta matokeo mazuri zaidi katika Elimu na kuwaongezea ujuzi wa maarifa mbali mbali ya teknolojia.

“Rai yangu kwenu kwa shule ya Kwiro, ni tuzipokee na tukazitunze kompyuta hizi ili ziwe na matokeo mazuri, viongozi wenzangu tuendelee kuiangalia shule hii vizuri, kwasababu ni shule inayotuheshimisha na inafanya vizuri ndani na nje ya Mkoa.” Amesema.

Amesema, kompyuta mpakato hizi, ni sehemu ya juhudi za dhati za Serikali inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuhakikisha maboresho ya Elimu yanaendelea nchini ili kupambana na changamoto ya ajira sambamba na kutengeneza kizazi bora cha baadae.

Nae, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania Dkt. Aneth Komba amesema,mwaka 2025 TET iliazimisha miaka 50, huku ikijiwekea malengo ya kuhakikisha upatikanaji wa vitabu na vifaa vya kufundishia kwa kidato cha kwanza mpaka cha nne, huku kwa kidato cha tano na sita kupata kompyuta moja kwa kila mwanafunzi.

Ameendelea kusema, kupitia lengo hilo TET iliendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Benki ya NMB kuhakikisha inafikia adhma hiyo ya kompyuta moja mwanafunzi mmoja kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita nchini ili kusaidia ujifunzaji na ufundishaji.

Kwa upande wake meneja wa NMB kanda ya kati Bi. Janeth Shango ameipongeza TET kwa jitihada inazofanya katika kuboresha elimu nchini hasa katika matumizi ya teknolojia katika kufundishia, hivyo kusisitiza NMB itaendelea kushirikiana na TET katika kutimiza ndoto za vijana katika eneo la elimu nchini.

Nae Mkuu wa shule ya Sekondari Kwiro Bw. John Kashamba ameishukuru TET, NMB na OWM TAMISEMI kwa kuchagua shule hiyo kuleta kompyuta hizo zitaongeza ari ya wanafunzi katika ujifunzaji na kwa walimu kufundishia kupitia MEWAKA , huku akisisitiza katika karne 21, TEHAMA ni kiungo muhimu katika ujenzi wa mfumo bora wa elimu.