Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Nishati, Bw. Petro Lyatuu akizungumza katika Kongamano la Siku ya Nishati (Energy Day) lililofanyika wakati wa Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba)

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Mhandisi Charles Sangweni akizungumza katika Kongamano la Siku ya Nishati (Energy Day) lililofanyika wakati wa Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba)

Mhandisi Mkuu wa Nishati, Bw. Christopher Nyondo, akizungumza katika Kongamano la Siku ya Nishati (Energy Day) lililofanyika wakati wa Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba)

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Nishati, Bi. Nteghenjwa Mbwambo, akiwakaribisha wageni na washiriki mbalimbali katika Kongamano la Siku ya Nishati (Energy Day) katika Ukumbi wa Mwandoro, Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere Sabasaba, jijini Dar es Salaam.

………..

NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM

Uwekezaji katika miundombinu ya sekta ya nishati unahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, sekta binafsi na taasisi za fedha ili kuhakikisha miradi mikubwa inapata rasilimali zinazohitajika na kutekelezwa kwa ufanisi.

Akizungumza katika Kongamano la Siku ya Nishati (Energy Day) lililofanyika wakati wa Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Nishati, Bw. Petro Lyatuu, amesema mafanikio ya miradi mikubwa ya nishati yanategemea uwepo wa mifumo imara ya ufadhili na ushirikiano wa wadau mbalimbali.

Amefafanua kuwa miradi ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme inahitaji mitaji mikubwa ambayo haiwezi kutegemea chanzo kimoja cha fedha.

Kutokana na hali hiyo, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuvutia wawekezaji pamoja na kushirikiana na taasisi za fedha ili kuwezesha utekelezaji wa miradi ya kimkakati.

Kwa mujibu wa Bw. Lyatuu, Serikali ina jukumu la kuweka mazingira wezeshi kupitia sera na mikakati inayochochea uwekezaji, huku taasisi za fedha zikisaidia upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Aidha, amesema maendeleo ya sekta ya nishati yanahitaji ushirikiano wa muda mrefu kati ya Serikali, sekta binafsi na washirika wa maendeleo, sambamba na upatikanaji wa rasilimali fedha za kutosha kwa ajili ya miradi ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme.

Ameongeza kuwa Tanzania ina fursa kubwa ya kuendeleza sekta ya nishati, hivyo ni muhimu kuimarisha mifumo ya kifedha, kuondoa vikwazo vya uwekezaji na kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ufanisi ili kuchochea maendeleo ya Taifa.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Mhandisi Charles Sangweni, alieleza mchango wa sekta ya mafuta na gesi asilia katika kukuza uchumi wa Taifa pamoja na umuhimu wa usimamizi madhubuti wa shughuli za mkondo wa juu wa petroli.

Mhandisi Sangweni alisisitiza haja ya kuendelea kuvutia uwekezaji, kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali, pamoja na kutumia kikamilifu fursa zilizopo katika sekta ya mafuta na gesi asilia kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mhandisi Mkuu wa Nishati, Bw. Christopher Nyondo, alieleza namna Wizara ya Nishati inavyotekeleza majukumu yake kwa kushirikiana na taasisi zilizo chini yake katika kusimamia maendeleo ya sekta hiyo nchini.

Bw. Nyondo alisema wizara inaendelea kuratibu shughuli za sekta, kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali na kuimarisha upatikanaji wa nishati ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Aidha, alibainisha kuwa ushirikiano kati ya Serikali, taasisi za nishati, sekta binafsi na wadau wengine ni muhimu katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya sekta hiyo.