Na Sixmund Begashe, Dodoma

VIONGOZI wa Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori wamepongeza kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii ya kuwainua wananchi kiuchumi kwa uwanzishwaji wa Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori (WMAs) nchini.

Akizungumza kwenye Kikao Kazi shirikishi cha kupokea maoni ya Rasimu ya Mwongozo wa Uanzishaji na Usimamizi wa WMAs kutoka kwa viongozi hao, Katibu Msaidizi wa Jumuiya Hifadhi ya Ngorongo, Utete na Mwaseni (JUHINGUMWA) iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji, Bw. Charles John Elimu, amesema mwongozo huo unakwenda kutoa dira kwenye Jumuiya zote, na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa shughuli za uhifadhi.

Bw. Elimu ameongeza kuwa mwongozo huo wa Serikali makini utasaidia kudhibiti matumizi mabaya ya fedha na kuwezesha fedha kutumika zaidi katika miradi ya maendeleo na hivyo kuongeza mapato ya jumuhia hizo.

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya WAGA iliyopo kati ya Halmashauri za Mufindi, Iringa na Mbarali Bi. Fatuma Mbembati, pamoja na kupongeza Serikali kwa jitihada zake za kuanzisha jumuhia hizo amesema mwongozo huo ukikamilika utasaidia kwenye usimamizi endelevu wa maliasili nchini na kuwakwamua wananchi kiuchumi.

Akifungua Kikao Kazi hicho kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Wizara ya Maliasili na Utalii, jijini Dodoma leo Julai 10, 2026, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara hiyo Bi. Kay Kagaruki amebainisha kuwa Wizara itaendelea kushirikiana na uongozi wa jumuiya hizo ili kuhakikisha migogoro ya kiutawala baina ya jumuiya zilizoidhinishwa na mamlaka nyingine za mitaa, malalamiko ya wananchi dhidi ya jumuiya ilyoidhinishwa yanamalizika kupitia Mwongozo unaoandaliwa na kuchechemua maendeleo ya kiuchumi, mshikamano wa kitaifa na amani chini.

Bi. Kagaruki amewataka washiriki hao kuhakikisha wanatoa vyema michango yao katika uandaaji wa Rasimu ya Mwongozi huo, kwa kuzingatia matamanio ya Wizara katika maendeleo ya jamii na uhifadhi unaoleta tabasamu kwa wananchi.