Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. James Kinyasi Millya (Mb.), ameambatana na ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ulioshiriki katika Maadhimisho ya 5 ya Siku ya Kiswahili Duniani yaliyofanyika jijini Bujumbura, Burundi, kutembelea Ofisi ya Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Burundi.
Wakati wa ziara hiyo, Mhe. Millya alipata fursa ya kusalimiana na Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Gelasius Byakanwa, pamoja na watumishi wa Ubalozi, na kupongeza kazi wanayoifanya katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Burundi.
Aidha, katika ziara hiyo Mhe. Millya ameambatana na Mhe. Hamis Mwinjuma (Mb.), Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo; Naibu Katibu Mkuu, Balozi Said S. Mussa; pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Miundombinu na Huduma za Jamii, Abdillah Mataka. Viongozi hao walitembelea na kukagua kiwanja cha Ubalozi kilichopo katika eneo la Melchior Ndadaye International Airport kwa lengo la kujionea milki za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Burundi.

