Kamishna wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Aretas James Lyimo, ameipongeza Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kwa mchango wake mkubwa katika kulinda afya ya wananchi kupitia usimamizi madhubuti wa ubora, usalama na ufanisi wa dawa pamoja na bidhaa nyingine za afya.
Kamishna Lyimo alitoa pongezi hizo alipotembelea banda la TMDA katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, ambapo alipata fursa ya kujionea huduma mbalimbali zinazotolewa na mamlaka hiyo pamoja na elimu inayotolewa kwa wananchi.
Katika ziara hiyo, Kamishna Lyimo alipokelewa na Meneja wa Kitengo cha Mawasiliano na Elimu kwa Umma wa TMDA, Gaudensia Simwanza, ambaye alimweleza kuhusu majukumu ya mamlaka hiyo katika kudhibiti ubora, usalama na ufanisi wa dawa, vifaa tiba, vitendanishi na bidhaa nyingine za afya, sambamba na juhudi za kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi sahihi ya dawa na umuhimu wa kutumia bidhaa za afya zilizosajiliwa.
Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo, Kamishna Lyimo alisema TMDA ina nafasi muhimu katika kuhakikisha bidhaa za afya zinazowafikia Watanzania zinakidhi viwango vinavyotakiwa, jambo ambalo linasaidia kulinda afya ya jamii na kuimarisha mapambano dhidi ya matumizi holela ya dawa.
Alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya TMDA na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ili kuongeza ufanisi katika kudhibiti matumizi mabaya ya dawa na bidhaa nyingine zinazoweza kutumika kinyume cha sheria.
Aidha, aliipongeza TMDA kwa kutumia Maonesho ya Sabasaba kama jukwaa la kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa elimu kuhusu matumizi salama ya dawa na bidhaa za afya, akieleza kuwa elimu hiyo ni muhimu katika kujenga jamii yenye afya na kupunguza athari zinazoweza kujitokeza kutokana na matumizi yasiyo sahihi ya dawa.

