Dar es Salaam. Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa, ameipongeza Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) kwa mageuzi inayoendelea kuyasimamia katika taasisi za umma, huku akiitaka kuendeleza juhudi hizo ili kuongeza tija ya uwekezaji wa Serikali.
Bw. Msigwa, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, alitoa pongezi hizo leo, Julai 8, 2026, alipotembelea banda la OTR katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
“Hongereni sana kwa mageuzi mnayofanya ambayo yamewezesha kuongezeka kwa gawio na michango mingine kutoka kwa taasisi za umma na kampuni ambazo serikali ina hisa chache. Endeleeni kufanya kazi hiyo kwa bidii zaidi,” alisema Bw. Msigwa alipotembelea banda la OTR lililopo Ukumbi wa Karume.
Kwa mwaka wa fedha 2025/26, OTR imekusanya jumla ya Sh1.327 trilioni kutoka katika mashirika ya umma na kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa hisa chache.
Kiasi hicho ni ongezeko la takribani Sh300 bilioni ikilinganishwa na Sh1.028 trilioni zilizokusanywa mwaka wa fedha 2024/25, sawa na ukuaji wa asilimia 30.
Aidha, Bw. Msigwa aliitaka OTR kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu uwekezaji wa Serikali wenye thamani ya Sh92.3 trilioni unaosimamiwa na Ofisi hiyo, uliowekezwa katika mashirika ya umma na kampuni ambazo Serikali ina hisa chache.
“Wananchi wanapaswa kujua kuwa uwekezaji huu ni mali yao. Hivyo, ni muhimu wauelewe na waulinde kwa maslahi ya Taifa,” alisema.
Aliongeza kuwa uelewa wa wananchi kuhusu uwekezaji wa Serikali utasaidia kuongeza uwajibikaji na kuthamini mchango wa taasisi za umma katika maendeleo ya nchi.
Gawio na michango mingine inayokusanywa kutoka kwa mashirika ya umma na kampuni ambazo Serikali ina hisa chache huwasilishwa katika Mfuko Mkuu wa Serikali, ambako hutumika kugharamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na utoaji wa huduma muhimu za kijamii, ikiwemo afya na elimu.
