Mkuu wa Wilaya ya Arusha ,Joseph Mkude akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ujio huo wa mwenge jijini Arusha kesho.
Na Happy Lazaro, Arusha 
Jumla ya miradi saba ya maendeleo yenye thamani ya Shilingi bilioni 3.9 inatarajiwa kuzinduliwa, kukaguliwa na kuwekewa jiwe  la msingi na Mbio za Mwenge wa Uhuru katika Halmashauri ya Jiji la Arusha.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, amesema Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kuwasili jijini Arusha kesho na kupokelewa  katika Viwanja vya Magereza jijini Arusha .
Mkude amesema baada ya mapokezi hayo, Mwenge wa Uhuru utaanza ziara ya kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo, ambapo utazindua, kukagua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi saba inayotekelezwa ndani ya Halmashauri ya Jiji la Arusha.
Ametaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa tenki la maji Kimindorosi, ujenzi wa chumba cha upasuaji katika Kituo cha Afya Moivaro na ujenzi wa shule ya ghorofa Muriet.
Miradi mingine itakayofikiwa na Mwenge wa Uhuru ni pamoja na ujenzi wa Barabara ya Giriki iliyopo Kata ya Sakina, mradi wa ufugaji wa kuku wa mayai na mradi wa uzalishaji wa chakula na uji unaoendeshwa na vijana.
Amesema miradi hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuboresha huduma za kijamii, kuimarisha miundombinu na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi kupitia uwekezaji katika sekta mbalimbali za maendeleo.
Mkude amewataka wananchi wa Jiji la Arusha kujitokeza kwa wingi kushiriki mapokezi ya Mwenge wa Uhuru na kushuhudia uzinduzi wa miradi hiyo, akisisitiza kuwa ushiriki wao ni muhimu katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuwaletea maendeleo.