Na Adelina Johnbosco – MAELEZO
Barabara za Mzunguko Jijini Dodoma imechangia kwa kiasi kikubwa kuondoa msongamano wa magari katikati ya jiji, hususan magari makubwa ya mizigo ya ndani na yanayokwenda nchi za nje.
Mradi huu wa barabara ya njia nne kwa kiwango cha lami una urefu wa jumla ya kilometa 112.3 huku sehemu ya kwanza (lot 1) yenye kilometa 52.3 ikiwa imekamilika kwa asilimia 93.3.
Barabara hii imeunganisha barabara kuu za mikoa minne, bandari kavu Ihumwa – Morogoro, Veyula – Arusha, Nala – Singida na Matumbulu – Iringa ambako sehemu ya pili ya ujenzi (lot 2) inaanzia.
Shughuli za usafiri na usafirishaji tayari zimeanza katika barabra hiyo, watumiaji wanashuhudia urahisi wa safari kutokana na kutokuwepo foleni.
“Imeturahisishia sana, inafanya safari iwe fupi kutokana na ukweli kwamba njia hii haina foleni hata kidogo kama kule mjini kati, mwanzoni kutoka Ihumwa hadi Nala ilikuwa tunatumia takribani saa na nusu hata zaidi, lakini kwa sasa tunatumia dakika 45 hadi 48 kwa safari hiyo hiyo” Bw. Simon Ndamanyilu, dereva lori
Akitoa ufafanuzi kuhusu barabara hiyo hivi karibuni, Mhandisi Morice Mlay, kutoka kampuni ya mzawa ya Inter-Consult Ltd (Mhandisi Mshauri wa Mradi), amesema barabara hiyo tayari imeanza kutumika na inatarajiwa kuzinduliwa rasmi Oktoba, 2026 ambapo itakuwa imekamilika kabisa.
“Ujenzi sehemu ya kwanza umefikia ukingoni, bado baadhi ya vitu vichache sana ikiwemo taa za barabarani na umaliziaji wa njia za watembea kwa miguu, magari mengi yanapita na yanapata urahisi kwa sababu hakuna foleni kwenye njia hii, mfano magari yanatoka moja kwa moja kutoka eneo la mzunguko wa Ihumwa hadi Nala ile barabara inayounganisha barabara ya Iringa bila kusimama popote” ametanabaisha Mha. Mlay
Barabara hiyo ya njia nne yenye njia mbili kila upande, zimetenganishwa na uwazi katikati kwa ajili ya matumizi mengine pindi itakapohitajika kuongeza miundombinu mingine au uboreshaji.
“Kuna baadhi ya watu wanashangaa kuhusu hili tuta lililoachwa katikati, hili ni kwa ajili ya matumizi ya baadaye mfano ujenzi wa barabara za mwendo kasi au kitu chochote kitakachoamuliwa kufanyika, lengo kuu ni kuepuka kutobomoa barabara kwa ajili ya kufanya kitu kipya” – Mha. Mlay
Baadhi ya wananchi jijini Dodoma wanaonesha furaha yao kutokana na uwepo wa barabara hiyo mpya inayopitisha magari mengi hasa magari makubwa ya mizingo kwenda ndani na nje ya nchi kwa wakati mmoja. Kwa mujibu wa Mha. Mlay, yapo magari yanayoelekea nchini Rwanda, Congo na Burundi kupitia barabara ya mzunguko.
Katika eneo la Nala ambako kuna mojawapo ya makutano ya barabara hiyo na sehemu ya maegesho ya magari, wakazi wa maeneo hayo wamepata fursa ya kufanya biashara kutokana na uwepo wa watu wengi kwa wakati mmoja.
“Kituo hiki yanapitisha na kusimama magari ya kila aina, hii ni tofauti na mwanzo, magari yakisimama hapa watu wanashuka na wengine wanakuwa wamesubiria kupanda, wengine ni madereva wa magari makubwa, kwa hiyo lazima watahitaji kupata mahitaji kutoka kwetu hasa chakula, hii ni furaha kwetu” Mary John, mama ntilie
Tamanio la wengi ni kuona barabara inaanza kazi rasmi kwani kwao ni tegemeo mojawapo la njia ya kuongeza kipato.
“Kama kwa sasa nauza bidhaa zangu kwa kiwango ambacho naona kinafaa, nawaza kwamba barabara hii ikianza kutumika rasmi magari yataongezeka, yataegeshwa kwa wingi zaidi na watu watakuwa wengi kuliko hivi” amesema Bi. Veronica Alfred, muuza nafaka eneo la Nala.
Mussa Rajab mkazi wa Nala na mkuli eneo hilo, akiwawakilisha wabeba mizigo wenzake, anasema uwepo wa sehemu ya kisasa ya kuegesha magari umefanya kazi yao kuwa rahisi na kukuza kipato.
“Mwanzoni eneo hili halikuwepo, hivyo kusimama kwa magari hapa ilitegemea udharura wa dereva hapo na sisi tunavizia kubeba mizigo japo kwa uchache sana, siku hizi magari yanasimama na mizigo inateremshwa hivyo tunabeba na kupata riziki” – Bw. Rajab
Mradi huu kipande cha kwanza utagharimu shilingi bil. 100.84 hadi kukamilika kwake, na unatarajiwa kuwa mwarobaini wa msongamano wa magari katikati ya jiji pia kukuza uchumi wa mkoa wa Dodoma, mikoa ya jirani na nchi kwa ujumla.
