Na John Bukuku, Dar es Salaam

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limewahimiza Watanzania kutembelea banda lake katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) ili kujionea teknolojia mbalimbali za kisasa zinazolenga kuongeza matumizi salama, nafuu na yenye ufanisi ya umeme katika maisha ya kila siku.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Viwanja vya Julius Nyerere, barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam Julai 4, 2026, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO, Irene Gowele amesema mwaka huu shirika hilo limekuja na maonesho tofauti yanayowapa wananchi fursa ya kujifunza matumizi ya teknolojia za kisasa za umeme.

“Kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, ninawakaribisha wananchi wote na wateja wetu kutembelea banda letu. Mbali na uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme, mwaka huu tunawaonesha Watanzania thamani ya matumizi ya umeme katika maisha yao ya kila siku,” alisema Gowele.

Amesema kivutio kikubwa ni Nyumba Janja (Smart Home), ambayo ina mfumo wa kisasa wa wiring ya kidijitali unaosaidia kuongeza usalama wa nyumba dhidi ya majanga kama moto pamoja na kuruhusu mmiliki kudhibiti matumizi ya vifaa vya umeme akiwa popote duniani kupitia simu ya mkononi.

Kwa mujibu wa Gowele, mfumo huo humwezesha mtumiaji kuwasha au kuzima vifaa vya umeme kwa kutumia programu maalumu na kufuatilia kiwango cha umeme kinachotumiwa na kila kifaa, hatua inayosaidia kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.

Aidha, amesema TANESCO inaendelea kuhamasisha matumizi ya vifaa vinavyotumia umeme kwa ufanisi (energy efficient), huku nyumba hiyo ikiwa imewekewa vifaa vinavyotumia kiwango kidogo cha umeme ili kuwasaidia wananchi kupunguza gharama za matumizi.

Gowele pia amewakumbusha wananchi kuhusu mpango wa TANESCO wa kukopesha majiko ya umeme, akisema wanaotembelea banda hilo wanaweza kuyapata kwa kununua au kwa mkopo kwa kutumia namba ya mita na Namba ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA) kwa ajili ya uhakiki.

Alillmesema majiko hayo ni ya matumizi yenye ufanisi mkubwa na yana uwezo wa kupika chakula cha Kitanzania kwa umeme wenye thamani ya chini ya shilingi 356, hivyo kuwa mbadala nafuu wa nishati nyingine za kupikia.

Katika maonesho hayo, wananchi pia wanapata fursa ya kujionea kwa teknolojia ya kidijitali miradi mikubwa ya TANESCO, ikiwemo Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere pamoja na Mradi wa Umeme wa Jua wa Kishapu mkoani Shinyanga unaozalisha megawati 50.

Pia amesema banda hilo linaelimisha wananchi kuhusu matumizi ya umeme katika sekta ya usafiri kupitia magari, pikipiki na bajaji zinazotumia umeme, akisisitiza kuwa Tanzania ina umeme wa kutosha hivyo wananchi wanapaswa kutumia fursa hiyo kupunguza gharama za usafiri na kulinda mazingira kwa kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa.

“TANESCO imekuja ki-smart Sabasaba mwaka huu. Tunawakaribisha wananchi wote waje wajifunze, wajionee teknolojia hizi na namna zinavyoweza kuboresha maisha yao huku zikipunguza gharama za matumizi ya nishati,” alisema Gowele.