NA DENIS MLOWE, IRINGA
MASHINDANO ya Great Ruaha Marathon yameendelea kujidhihirisha kuwa jukwaa muhimu la kutangaza utalii wa kusini mwa Tanzania, kuhamasisha uhifadhi wa mazingira pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia michezo, huku viongozi mbalimbali wakitoa wito wa kulinda Mto Ruaha Mkuu na rasilimali za asili zinazotegemewa na mamilioni ya Watanzania.
Akifunga mashindano hayo, mgeni rasmi Nehemia Mchechu alisema Great Ruaha Marathon si mashindano ya riadha pekee, bali ni jukwaa linalounganisha michezo, afya, utalii, uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya vijana.
Mchechu alisema Tanzania bado ina fursa kubwa ya kukuza uchumi kupitia sekta ya utalii ikiwa vivutio vya asili vitatumika ipasavyo kuvutia wageni, wawekezaji na kuongeza ajira kwa wananchi.
Alisema Mto Ruaha Mkuu una umuhimu mkubwa katika uhifadhi wa mazingira, uzalishaji wa umeme, kilimo na maisha ya wananchi, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kulinda vyanzo vya maji, kupanda miti na kutumia rasilimali za asili kwa uwajibikaji ili kuhakikisha vizazi vijavyo vinaendelea kunufaika.
Aliwataka wananchi kuendelea kushiriki shughuli za michezo kwa kuwa ni njia muhimu ya kuboresha afya na kuongeza tija katika maendeleo ya taifa, huku akiwapongeza waandaaji kwa kufanikisha miaka mitano ya mashindano hayo ambayo amesema ni mafanikio makubwa.
Mchechu pia aliipongeza Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), wadhamini na washirika mbalimbali kwa kuendelea kuunga mkono mashindano hayo yenye upekee wa kufanyika ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, akisema hali hiyo inaipa Tanzania nafasi ya kipekee katika soko la utalii duniani.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamini Sitta, alisema pamoja na mafanikio ya marathon hiyo, bado kuna changamoto ya uwindaji haramu na uharibifu wa mazingira unaotishia uhai wa Mto Ruaha Mkuu na hifadhi ya taifa.
Alisema kupungua kwa kiwango cha maji katika mto huo kunatokana na uharibifu wa mazingira kwenye maeneo ya vyanzo vya maji, jambo linaloweza kuathiri uhifadhi wa wanyamapori pamoja na uzalishaji wa umeme katika mabwawa ya Mtera na Julius Nyerere.
Sitta aliwataka wananchi wanaoishi kandokando ya mto huo kushiriki kikamilifu katika juhudi za kuhifadhi mazingira ili kuhakikisha mto unaendelea kuwa chanzo cha maji kwa binadamu, wanyamapori na shughuli za uzalishaji wa nishati.
Naye Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Cosato Chumi, alisema Great Ruaha Marathon imekuwa nyenzo muhimu ya kuitangaza Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na utalii wa ukanda wa kusini, huku ikivutia washiriki kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Alisema kupitia mashindano hayo serikali inaendelea kufikia lengo la kuongeza idadi ya watalii, mapato ya fedha za kigeni pamoja na ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa wananchi.
Chumi aliongeza kuwa pamoja na kukuza utalii, marathon hiyo imeendelea kuimarisha umoja wa Watanzania na wageni kutoka mataifa mbalimbali, huku ikitoa fursa za biashara kwa wajasiriamali wanaouza bidhaa na huduma mbalimbali wakati wa mashindano.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa SYDP Edward Milinga ambao ni waandaaji wa Great Ruaha Marathon, aliwashukuru viongozi wa Serikali ya Mkoa wa Iringa, wadhamini, washirika na timu ya waandaaji kwa mchango wao mkubwa uliowezesha kufanikisha msimu wa tano wa mashindano hayo.
Alisema ushirikiano uliopo kati ya waandaaji, serikali na wadau mbalimbali umeendelea kuifanya Great Ruaha Marathon kukua kila mwaka, huku akieleza kuwa wataendelea kubuni njia mpya za kuitangaza kimataifa ili kuongeza idadi ya washiriki na watalii wanaotembelea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.