Zaidi ya wananchi 1,940 wamepatiwa huduma za bure za uchunguzi wa macho katika Banda la Mixx by Yas kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), huku watu 41 wakigundulika kuwa na tatizo la mtoto wa jicho na kupewa rufaa ya kufanyiwa upasuaji bila gharama.
Mtaalamu wa Macho na Afya ya Jamii kutoka Taasisi ya Bilal Muslim Patrick Martine, amesema mwitikio wa wananchi umekuwa mkubwa tangu huduma hizo zilipoanza Julai 1, huku wengi wakibainika kuwa na matatizo ya kutokuona mbali, kutokuona karibu na aleji za macho.
Amesema watu 41 waliogundulika kuwa na mtoto wa jicho watapatiwa upasuaji bure kupitia Bilal Muslim Mission of Tanzania, huku wengine wakipatiwa dawa na miwani bila malipo.
Martine amesema matumizi makubwa ya vifaa vya kidijitali kwa watoto na kukosa muda wa kucheza nje ni miongoni mwa sababu zinazochangia ongezeko la matatizo ya macho, akiongeza kuwa kusitishwa mapema kwa unyonyeshaji wa maziwa ya mama pia kunatajwa na tafiti kuwa miongoni mwa sababu zinazoweza kuchangia changamoto hiyo.
Mwananchi aliyepata huduma hiyo, Cecilia Wilson wa Mtoni Kijichi, amesema amefurahishwa na huduma hiyo baada ya kupimwa macho na kupewa miwani miwili bila kulipa chochote, huku akiwahimiza Watanzania wenye changamoto za macho kufika katika Banda la YAS kupata huduma hizo za bure.
Kwa upande wake, Meneja wa Banda la Mixx by Yas, Omega Mwakifuna, amesema utoaji wa huduma za macho ni sehemu ya mpango wa kampuni wa kurudisha kwa jamii. Amesema kutokana na mwitikio mkubwa wa wananchi, mwaka huu huduma hizo zinatolewa kwa siku saba kuanzia Julai 1 hadi 7, ambapo wananchi wanapata vipimo, ushauri wa kitaalamu, dawa na miwani bila malipo.
