Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Mheshimiwa Daniel Francisco Chapo akihutubia kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam tarehe 03 Julai, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akimkabidhi zawadi mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Mheshimiwa Daniel Francisco Chapo katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam, tarehe 03 Julai, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa na Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Mheshimiwa Daniel Francisco Chapo wakitembelea Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam, tarehe 03 Julai, 2026.

………….. 

Na John Bukuku, Dar es Salaam.

Rais wa Msumbiji, , amesema Tanzania ina nafasi ya kipekee katika mioyo na kumbukumbu za wananchi wa Msumbiji kutokana na mchango wake mkubwa katika harakati za ukombozi wa taifa hilo, akieleza kuwa ardhi ya Tanzania ndiyo iliyokuwa chimbuko la mapambano yaliyozaa uhuru wa Msumbiji.

Rais Chapo aliyasema hayo Julai 3, 2026, alipokuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) yaliyofanyika katika Viwanja vya Sabasaba, Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam, ambapo aliambatana na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Kwa sababu hiyo, Tanzania ina nafasi ya kipekee katika mioyo na kumbukumbu za wananchi wa Msumbiji. Ni katika ardhi hii yenye ukarimu ambapo wapigania uhuru wetu wengi walipata hifadhi. Ni hapa ndipo FRELIMO ilipopata msaada wa kisiasa, kidiplomasia na kibinadamu uliowezesha kuandaa mapambano yaliyotufikisha kwenye uhuru wa taifa letu. Kwa hiyo, tunaweza kusema kwamba Tanzania ndiyo chimbuko la uhuru wa Msumbiji,” alisema.

Alisisitiza kuwa wananchi wa Msumbiji hawatasahau kamwe mchango wa Tanzania katika kipindi ambacho uhuru ulikuwa bado ndoto, akisema Tanzania iliigeuza ndoto hiyo kuwa mapambano ya pamoja yaliyowezesha taifa hilo kupata uhuru.

Rais Chapo alisema urafiki kati ya Tanzania na Msumbiji haukujengwa kwa misingi ya biashara au maslahi ya kiuchumi pekee, bali ulijengwa juu ya ujasiri, mshikamano, kujitolea na imani kwamba uhuru wa taifa moja la Afrika ni ushindi wa bara lote.

Alikumbusha kuwa kabla ya mataifa hayo mawili kuingia katika makubaliano rasmi ya ushirikiano, tayari wananchi wake walikuwa wakitembea bega kwa bega wakipigania uhuru, wakiongozwa na waasisi wa mataifa hayo, na .

“Msumbiji na Tanzania havijaunganishwa na historia pekee. Sisi si washirika wa kiuchumi tu, bali ni wenzetu katika mapambano ya ukombozi wa taifa,” alisema.

Rais Chapo alisema kizazi cha sasa kina wajibu wa kuendeleza urithi huo kwa kuhakikisha kinapigania uhuru wa kiuchumi wa Afrika, kama ambavyo waasisi wa mataifa hayo walivyopigania uhuru wa kisiasa.

Alisema ni wakati wa kuigeuza mipaka ya kijiografia kuwa njia za ustawi wa pamoja kwa kujenga uchumi uliounganishwa, wenye ushindani na unaotoa fursa kwa wananchi, hususan vijana na wanawake.

“Kama wao walivunja minyororo ya ukoloni na mipaka iliyotugawa, sisi tunapaswa kuigeuza mipaka ya kijiografia kuwa njia za ustawi na maendeleo kwa manufaa ya wananchi wetu,” alisema.

Rais huyo alisema uchumi wa Tanzania na Msumbiji unakamilishana badala ya kushindana, jambo linalotoa msingi imara wa kuongeza biashara, uwekezaji na maendeleo ya pamoja.

Alibainisha kuwa kuongezeka kwa imani ya sekta binafsi pamoja na kazi inayofanywa na Tume ya Pamoja ya Ushirikiano wa Nchi Mbili kumeendelea kuimarisha uhusiano wa kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili.

Aidha, alisisitiza dhamira ya Serikali ya Msumbiji kuendelea kushirikiana kwa karibu na Tanzania katika kujenga eneo la kiuchumi lililounganishwa zaidi kwa manufaa ya wananchi wa nchi hizo mbili.

Akizungumzia Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam, Rais Chapo alisema yamejidhihirisha kuwa miongoni mwa majukwaa makubwa ya biashara na uwekezaji Afrika Mashariki, akiyataja kuwa chachu ya uzalishaji, ubunifu, viwanda na maendeleo ya kiuchumi kwa zaidi ya nusu karne.

Pia aliwataka wafanyabiashara wa Tanzania na wawekezaji wa kimataifa kushiriki Maonesho ya Sita ya Kimataifa ya Maputo yatakayofanyika mwishoni mwa Agosti hadi mwanzoni mwa Septemba mwaka huu, akisema yatakuwa fursa nyingine ya kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Msumbiji.

Akihitimisha hotuba yake, Rais Chapo alisema Afrika inapaswa kuiona mipaka yake ya kisiasa kama mipaka ya kiutawala pekee, huku katika biashara na uchumi ikijiona kama soko moja lenye historia, tamaduni na malengo yanayofanana ya kujiletea maendeleo na ustawi kwa wananchi wake.