Na John Bukuku Dar es Salaam

Julai 3, 2026, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba, ametangaza kuongezeka kwa Riba ya Benki Kuu (CBR) kutoka asilimia 5.75 hadi asilimia 6.25 kwa robo mwaka unaoishia Septemba 2026, hatua inayolenga kudhibiti mfumuko wa bei unaochochewa na kupanda kwa bei za mafuta, mbolea na gharama za usafirishaji duniani.

Akizungumza Julai 3, 2026 katika makao makuu ya Benki Kuu jijini Dar es Salaam, Gavana Tutuba alisema uamuzi huo ulifikiwa na Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) katika kikao chake kilichofanyika Julai 2, 2026, baada ya kutathmini mwenendo wa uchumi wa dunia na wa ndani.

Alisema ongezeko hilo la riba linalenga kuhakikisha mfumuko wa bei unaendelea kubaki ndani ya lengo la asilimia 3 hadi 5 huku ukiunga mkono ukuaji endelevu wa shughuli za uchumi nchini.

Tutuba alisema pamoja na changamoto zinazosababishwa na mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati, bei za chakula zinatarajiwa kupungua kutokana na mavuno mazuri ya msimu wa kilimo wa mwaka 2025/26. Aidha, alieleza kuwa uimara unaotarajiwa wa thamani ya shilingi utachangiwa na ongezeko la mapato yatokanayo na mauzo ya dhahabu, mazao ya kilimo na shughuli za utalii, hali itakayosaidia kupunguza gharama za bidhaa zinazoagizwa kutoka nje.

Kwa mujibu wa tathmini ya Kamati, uchumi wa dunia umepungua kasi katika robo mwaka iliyoishia Juni 2026 kutokana na athari za mgogoro wa Mashariki ya Kati uliovuruga usambazaji wa mafuta na njia muhimu za biashara. Hali hiyo imeongeza bei za mafuta ghafi, mbolea na gharama za usafirishaji, na hivyo kuongeza mfumuko wa bei duniani.

Hata hivyo, Kamati imesema uchumi wa Tanzania umeendelea kuhimili misukosuko hiyo, huku uchumi wa Tanzania Bara ukikadiriwa kukua kwa asilimia 6 katika nusu ya kwanza ya mwaka 2026, ukichochewa na sekta za kilimo, ujenzi, madini, huduma za kifedha na usafirishaji.

Kwa upande wa Zanzibar, uchumi unakadiriwa kukua kwa asilimia 6.6 kutokana na kuimarika kwa shughuli za utalii na ujenzi, huku matarajio yakionesha uchumi wa nchi utaendelea kukua kwa zaidi ya asilimia 6 katika nusu ya pili ya mwaka huu.

Katika upande wa mfumuko wa bei, Gavana alisema Tanzania Bara uliongezeka hadi asilimia 4.2 mwezi Mei 2026 kutoka asilimia 3.2 mwezi Machi, lakini umeendelea kubaki ndani ya kiwango kinacholengwa. Aliongeza kuwa ruzuku ya mafuta iliyotolewa na Serikali katika miezi ya Mei na Juni ilisaidia kupunguza kasi ya ongezeko hilo.

Aidha, alisema sekta ya fedha imeendelea kuwa imara, huku mikopo kwa sekta binafsi ikikua kwa wastani wa asilimia 24 na uwiano wa mikopo chechefu kubaki katika asilimia 2.9 mwezi Mei 2026, chini ya kiwango kinachokubalika cha asilimia 5.

Katika sekta ya nje, alisema akiba ya fedha za kigeni imefikia dola za Marekani bilioni 6, kiwango kinachotosha kugharamia uagizaji wa bidhaa na huduma kwa miezi 4.3, juu ya lengo la taifa la angalau miezi minne.

Gavana Tutuba alisema Kamati ya Sera ya Fedha itaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa uchumi wa dunia na wa ndani ili kuhakikisha utulivu wa bei unaendelea kuwepo nchini.

Alitangaza kuwa kikao kijacho cha Kamati ya Sera ya Fedha kitafanyika Oktoba 7, 2026, ambapo uamuzi wa Riba ya Benki Kuu kwa robo ya nne ya mwaka 2026 utatangazwa siku inayofuata.