Kutoka kushoto ni Ami R. Mpungwe (Mwenyekiti wa Mpito wa Bodi ya Tanzania Breweries PLC), Michelle Kilpin, Mtendaji Mkuu wa TBL (Katikati) akizungumza na wanahisa katika Mkutano Mkuu wa Wanahisa, ambapo wanahisa wamepitisha taarifa ya fedha ya mwaka wa mapato wa 2025/2026 kufuatia ukuaji wa faida uliotangazwa. Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Fedha TBL, Avito Swai
……………
Na John Bukuku
Dar es Salaam. Wanahisa wa Tanzania Breweries PLC wamepitisha Ripoti ya Wakurugenzi, Ripoti ya Wakaguzi wa Hesabu pamoja na taarifa za fedha zilizokaguliwa kwa mwaka ulioishia Desemba 31, 2025, kufuatia mwaka ulioshuhudia ukuaji mkubwa wa mapato na faida za kampuni.
Uamuzi huo ulifikiwa katika Mkutano Mkuu wa 53 wa Wanahisa uliofanyika Julai 2, 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam, ambapo wanahisa wengine walishiriki kwa njia ya mtandao. Mkutano huo pia ulithibitisha mgao wa muda (interim dividend) uliolipwa kwa mwaka 2025 na kuidhinisha kampuni ya PricewaterhouseCoopers kuwa wakaguzi wa hesabu wa nje kwa mwaka wa fedha 2026.
Kwa mujibu wa taarifa ya kampuni, TBL ilirekodi ongezeko la asilimia 13 ya mapato na asilimia 35 ya faida ya uendeshaji mwaka 2025, mafanikio yaliyotokana na kuongezeka kwa mahitaji ya bia na vileo vikali, usimamizi madhubuti wa gharama, uwekezaji katika chapa pamoja na kuboresha mfumo wa usambazaji wa bidhaa.
Mwenyekiti wa Muda wa Bodi ya Wakurugenzi wa TBL, Ami R. Mpungwe, alisema Mkutano Mkuu wa Wanahisa unaendelea kuwa jukwaa muhimu la uwajibikaji na uwazi, huku Bodi ikiendelea kulinda maslahi ya wanahisa na kuisimamia kampuni ili iendelee kukua kwa uwajibikaji na kuchangia maendeleo ya uchumi wa Tanzania.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TBL, Michelle N. Kilpin, alisema matokeo ya mwaka 2025 yamechochewa na uimara wa chapa za kampuni, utekelezaji wenye nidhamu na imani ya wateja na wanahisa. Alisema kampuni itaendelea kuwekeza katika chapa zake, kuimarisha mifumo ya kidijitali, kuongeza matumizi ya malighafi za ndani na kuboresha ufanisi wa shughuli zake.
Mbali na mafanikio ya kifedha, TBL iliendelea kuimarisha mchango wake katika uchumi wa ndani kupitia Kiwanda cha Kimea cha Kilimanjaro chenye uwezo wa kuzalisha tani 8,000 za kimea kwa mwaka, hatua inayoongeza matumizi ya shayiri inayolimwa nchini. Kampuni pia imeendelea kuwaunga mkono wakulima wa shayiri na mtama, kupanua mfumo wa kidijitali wa kuagiza bidhaa na kuimarisha ushirikiano na wafanyabiashara wa rejareja.
Katika eneo la uendelevu, TBL ilieleza kuwa asilimia 92 ya vifungashio vyake vinaweza kurejeshwa au kutengenezwa kutokana na malighafi zilizorejelewa, huku matumizi ya maji yakiendelea kuboreshwa. Kampuni ilisisitiza itaendelea kukuza biashara kwa uwajibikaji, kujenga thamani kwa wanahisa na kuendelea kuchangia maendeleo ya uchumi wa Tanzania.

