Matumizi mabaya ya dawa tiba zenye asili ya kulevya yameelezwa kuwa miongoni mwa vyanzo vinavyochochea ongezeko la uraibu, uhalifu na athari mbalimbali za kiafya pale dawa hizo zinapochepushwa kutoka katika matumizi yake halali ya kitabibu na kutumiwa kutengeneza au kuchanganywa na dawa za kulevya.
Hayo yameelezwa na Kamishna Msaidizi wa Sayansi Jinai wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Ziliwa Peter Machibya, wakati akiwasilisha mada katika semina ya waandishi wa habari iliyofanyika katika Ukumbi wa Makumbusho, jijini Dar es Salaam, Julai 3, 2026.
Machibya amesema ni muhimu jamii kutambua kuwa dawa tiba zenye asili ya kulevya si dawa za kulevya zenyewe, bali ni dawa halali zinazotumika katika huduma za afya kwa madhumuni ya matibabu chini ya usimamizi wa wataalamu wa afya. Amesema tatizo huanza pale dawa hizo zinapochepushwa kutoka kwenye matumizi yake halali na kutumiwa kutengeneza au kuchanganywa na dawa za kulevya.
“Dawa tiba zenye asili ya kulevya si dawa za kulevya. Hizi ni dawa halali zinazotumika hospitalini kwa ajili ya matibabu. Changamoto inaanza pale zinapochepushwa na kutumiwa vibaya kutengeneza au kuchanganywa na dawa za kulevya,” amesema Machibya.
Amesema matumizi hayo mabaya husababisha uraibu, ambapo mtumiaji hupata hamu kubwa ya kuendelea kutumia dawa hizo licha ya madhara yanayomtokea. Aidha, huweza kusababisha utegemezi, hali ambayo mwili na akili hushindwa kufanya kazi kawaida bila matumizi ya dawa hizo na hivyo kumfanya mtumiaji ashindwe kuziacha.
Machibya amesema matumizi mabaya ya dawa hizo pia husababisha madhara makubwa ya kiafya, ikiwemo kuharibika kwa mifumo mbalimbali ya mwili, kuongezeka kwa matatizo ya afya ya akili, kupungua kwa uwezo wa kupumua, kuvimbiwa, kupoteza hamu ya kula, kubadilika kwa hisia na mwenendo, pamoja na kusababisha vifo vya ghafla.
Aidha, amesema matumizi hayo ni hatari zaidi kwa wajawazito kwa kuwa yanaweza kusababisha kuharibika kwa mimba, kujifungua watoto wenye uzito mdogo na kuathiri afya ya kizazi kijacho, jambo linaloifanya changamoto hiyo kuwa ya kizazi hadi kizazi.
Kwa upande wa athari za kijamii, Machibya amesema uchepushaji wa dawa tiba zenye asili ya kulevya huchochea vitendo vya uhalifu kama vile ubakaji, mauaji, utekaji na utapeli, huku pia ukiongeza ajali, vifungo na biashara haramu ya dawa za kulevya. Amesema hali hiyo hupunguza pia imani ya wananchi kwa taasisi zinazohusika na udhibiti wa dawa.
Amesema uchumi wa taifa nao huathirika kutokana na kupungua kwa ushindani wa biashara, kuvurugika kwa mnyororo wa usambazaji wa dawa muhimu na kuongezeka kwa ugumu wa upatikanaji wa dawa kwa wagonjwa wanaozihitaji kwa matumizi halali. Vilevile, Serikali hulazimika kutumia fedha nyingi kugharamia matibabu ya waraibu na waathirika pamoja na kuendesha operesheni na ukaguzi maalumu wa kukabiliana na tatizo hilo.
Machibya ametoa wito kwa wananchi kutumia dawa tiba zenye asili ya kulevya kwa kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya na kuhakikisha hazichepushwi kwa matumizi yasiyo halali. Aidha, amewataka waandishi wa habari kuendelea kuielimisha jamii kuhusu madhara ya uchepushaji wa dawa hizo na umuhimu wa kushirikiana na DCEA katika kuzuia matumizi mabaya yanayochochea uzalishaji na matumizi ya dawa za kulevya.

