Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba ameagiza bidhaa zilizochukuliwa kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara wadogo wa Tarafa ya Shelui, Wilaya ya Iramba mkoani Singida kurejeshwa mara moja na kuwataka watendaji wa taasisi za udhibiti kuacha kuchukua mitaji ya wananchi wakati wa utekelezaji wa shughuli za ukaguzi.

Dkt. Mwigulu ametoa maelekezo hayo leo, Jumamosi Juni 13, 2026, alipokuwa akizungumza, kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi wa Tarafa ya Shelui katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Mnadani, Kata ya Mgongo, Wilaya ya Iramba.

Ametoa agizo hilo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara wadogo waliodai kuchukuliwa kwa mafuta yao na baadhi ya watendaji wa taasisi za udhibiti, hali iliyowaathiri katika shughuli zao za kujipatia kipato.

Akizungumza kuhusu suala hilo, Waziri Mkuu alihoji sababu za kuchukuliwa kwa bidhaa hizo na kusisitiza kuwa Serikali haitaki kuona wananchi wanaojitafutia kipato kupitia biashara ndogo ndogo wakinyang’anywa mitaji yao.

“Ulikuwa unafuatilia ziara za Waziri Mkuu? Nilisemaje kuhusu kuchukua bidhaa za wananchi? Kwa nini mmechukua? Huo ni mtaji wake. Dumu moja la mafuta ndiyo mtaji wake. Nimewaambia msikamate hata bakuli la maharage, nyinyi kwa nini mmeenda kuchukua mafuta yao?” amesema Dkt. Mwigulu.

Aidha, aliagiza bidhaa hizo kurejeshwa mara moja kwa wahusika.

“Itarudishwa leo leo. Muwatafute leo leo muwarudishie bidhaa zao. Nimeshaelekeza yarudishwe leo leo na waendelee na shughuli zao,” amesema.

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwataka watendaji wote wanaosimamia shughuli za udhibiti nchini kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo bila kuathiri shughuli halali za kiuchumi za wananchi.

“Narejea tena, watu wote mnaosimamia mambo ya udhibiti, msichukue bidhaa za wananchi. Hizo ni ofisi zao, hiyo ni mitaji yao. Msichukue bidhaa za wananchi, msichukue bidhaa za Watanzania. Hizo ni ofisi zao,” amesema.

Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu amesema Serikali itaendelea kuimarisha huduma za maji nchini kupitia utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria, miradi ya miji 28 pamoja na miradi ya visima kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa Mkoa wa Singida na maeneo mengine nchini.

Amesema miradi hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za maji na kupunguza changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo katika maeneo mbalimbali nchini.

“Tunao mradi huu wa kutokea Ziwa Victoria, tunao mradi wa visima, tunao mradi wa miji 28. Miradi yote hii inalenga kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama. Kabla maji ya Ziwa Victoria hayajafika Dodoma, yatakuwa yameshasambaa katika vijiji mbalimbali vya Wilaya ya Iramba pamoja na maeneo mengine ya Mkoa wa Singida,” amesema.

Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kufuatilia utekelezaji wa miradi hiyo katika mwaka mpya wa fedha ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji kwa uhakika zaidi.

Kuhusu huduma za afya, Dkt. Mwigulu ameagiza kupelekwa kwa gari la wagonjwa (ambulance) katika Tarafa ya Shelui ndani ya wiki mbili ili kuboresha huduma za dharura kwa wananchi wa eneo hilo.

“Ndani ya wiki hizi mbili tutakuwa tumeleta gari la wagonjwa katika Tarafa ya Shelui. Hivi tunavyoongea dereva wa kwenda kulichukua yuko Dar es Salaam. Kwa hiyo ambulance itakuja ili tumalize changamoto hii ambayo wananchi wameiwasilisha,” amesema.

Aidha, amesema Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya afya ikiwemo Kituo cha Afya Mgongo pamoja na kuendeleza mipango ya ujenzi wa miundombinu mingine ya afya katika wilaya hiyo.

Akizungumzia miundombinu ya barabara, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea na usanifu wa miradi mbalimbali ya barabara na madaraja ili kuboresha mawasiliano na kurahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Wilaya ya Iramba na maeneo jirani.

Wakati huo huo, Dkt. Mwigulu ameagiza viongozi wa Wilaya ya Iramba pamoja na mamlaka husika kukutana na wadau wa sekta ya madini ili kujadili changamoto zilizowasilishwa na wachimbaji wadogo na kutafuta suluhisho litakalolinda maslahi ya wananchi, wawekezaji na Serikali.

“Kesho tukutane tujadili kwa pamoja. Tutawasikiliza wote ili tuweze kupata suluhisho ambalo litalinda maslahi ya wananchi wetu na wakati huo huo kuendeleza uwekezaji,” amesema.