Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali imewasilisha bungeni mapendekezo yatakayowezesha fedha za miradi ya maendeleo katika sekta za maji, barabara na nishati kupelekwa moja kwa moja kwenye mifuko husika ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Dkt. Mwigulu amesema hayo leo, Jumamosi Juni 13, 2026, alipokuwa akizungumza na wananchi wa Tarafa ya Ndago katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Ndago, Wilaya ya Iramba mkoani Singida.
Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha fedha zinazotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi zinafika moja kwa moja katika sekta husika na kuwezesha utekelezaji wa miradi kufanyika kwa ufanisi na kwa wakati.
“Fedha zote zinazokwenda kwenye barabara, maji na umeme hazitapita tena kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Zitakwenda moja kwa moja kwenye mifuko husika ili kuhakikisha utekelezaji wa miradi unaongezeka kasi,” amesema Dkt. Mwigulu.
Waziri Mkuu amesema hatua hiyo itaongeza kasi ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo utekelezaji wake ulipungua katika kipindi kilichopita kutokana na Serikali kuelekeza rasilimali nyingi katika kukamilisha miradi mikubwa ya kimkakati ya Taifa.
Ametaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), Daraja la Kigongo–Busisi pamoja na Reli ya Kisasa (SGR), ambayo kwa sasa imekamilika au imefikia hatua kubwa za utekelezaji.
“Tulifanya uamuzi wa kimkakati na wa kizalendo wa kukamilisha miradi hiyo kwa sababu ilikuwa muhimu kwa mustakabali wa Taifa. Sasa miradi hiyo imekamilika au imefikia hatua kubwa za utekelezaji na hivyo kasi ya utekelezaji wa miradi mingine itaongezeka,” amesema.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu amesema Serikali itaongeza kasi ya utekelezaji wa mradi wa Barabara ya Kizaga–Ndago–Sepuka–Singida, ambayo ni miongoni mwa miradi muhimu ya miundombinu inayounganisha maeneo makubwa ya uzalishaji wa mazao katika Wilaya ya Iramba.
Amesema Serikali inatambua umuhimu wa barabara hiyo katika kuchochea shughuli za uzalishaji, biashara na usafirishaji wa mazao hususan katika Tarafa za Ndago na Shelui ambazo ni miongoni mwa maeneo yanayoongoza kwa uzalishaji katika wilaya hiyo.
“Barabara hii ni muhimu sana kwa wananchi wetu. Ni barabara inayounganisha maeneo makubwa ya uzalishaji na ndiyo maana Serikali imeendelea kuipa kipaumbele katika mipango yake ya maendeleo,” amesema.
Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya madaraja katika maeneo mbalimbali ya Tarafa ya Ndago ili kuondoa changamoto za usafiri na usafirishaji, hususan katika maeneo yanayoathirika wakati wa mvua.
Amesema katika mwaka wa fedha unaoanza Julai 1, 2026, Serikali itaanza utekelezaji wa miradi mbalimbali ya madaraja pamoja na usanifu wa madaraja makubwa yatakayorahisisha mawasiliano na kuimarisha usalama wa wananchi.
Sambamba na hilo, Dkt. Mwigulu amesema Serikali inaendelea na hatua za kuendeleza kilimo cha umwagiliaji katika Bonde la Dengu kupitia usanifu wa miundombinu ya mabwawa na mifumo mingine ya kuhifadhi maji kwa ajili ya kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao.
“Usanifu unaendelea katika Bonde la Dengu ili tuweze kuwa na miundombinu ya umwagiliaji itakayowezesha wananchi kuongeza uzalishaji na tija katika kilimo,” amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali imeanza kutafuta suluhisho la kudumu la changamoto zinazowakabili wakulima katika mfumo wa stakabadhi ghalani kwa kuongeza uwekezaji katika ujenzi wa maghala kwenye maeneo ya uzalishaji.
Amesema hatua hiyo itapunguza gharama za usafirishaji wa mazao, kurahisisha uhifadhi wa mazao na kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa mfumo wa stakabadhi ghalani.
“Tutajenga maghala katika maeneo ya uzalishaji wa mazao yanayotumia mfumo wa stakabadhi ghalani ili kupata suluhisho la kudumu la changamoto hii,” amesema.
Wakati huo huo, Dkt. Mwigulu ametangaza kupelekwa kwa gari jipya la wagonjwa (ambulance) katika Tarafa ya Ndago ndani ya wiki moja hadi mbili ili kuimarisha huduma za rufaa na dharura kwa wananchi wa eneo hilo.
Amesema ambulance hiyo itasaidia kuhudumia wananchi wa maeneo mbalimbali ya tarafa hiyo na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za afya.
“Ndani ya wiki moja hadi mbili ambulance mpya itakuwa imefika Ndago kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wa tarafa hii,” amesema.

