Na John Bukuku, Dar es Salaam.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo, amewataka wananchi wanaotaka kununua viwanja na ardhi kuhakikisha wanapata ushauri kutoka kwa wataalamu wa ardhi kabla ya kufanya manunuzi ili kuepuka migogoro ya umiliki.

Akizungumza katika Banda la Wizara ya Ardhi kwenye Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Dkt. Akwilapo alisema wananchi wengi huingia kwenye migogoro kwa kununua ardhi bila kuthibitisha umiliki wake kupitia ofisi za ardhi.

“Ardhi si kitu cha kwenda kujichotea ovyo. Kabla ya kununua kiwanja, nenda ofisi za ardhi upate ushauri wa wataalamu. Watahakiki eneo husika na kukueleza kama lina mgogoro au la,” alisema.

Aliongeza kuwa baadhi ya viongozi wa mitaa au vijiji hutoa taarifa ambazo wakati mwingine si sahihi, hivyo wananchi wanapaswa kuthibitisha taarifa zote katika ofisi rasmi za ardhi.

Dkt. Akwilapo alisema wizara imeendelea kuboresha mifumo ya utoaji wa hati ili kuondoa changamoto ya kiwanja kimoja kupewa hati zaidi ya moja.

“Sasa hivi mifumo yetu imeboreshwa. Mfumo ukishatoa hati kwa mtu mmoja hauwezi kutoa hati nyingine kwa kiwanja hicho, hivyo tatizo la hati mbili katika kiwanja kimoja litakuwa historia,” alisema.

Aidha, alisema maeneo mengi ya makazi yasiyopangwa bado ni changamoto kubwa katika ukuaji wa miji, hususan Dar es Salaam, na wizara inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kutafuta fedha za kupima maeneo mengi zaidi ili wananchi wapate viwanja vilivyopangwa rasmi.

Kwa upande wa huduma zinazotolewa katika Maonesho ya Sabasaba, Dkt. Akwilapo alisema mwitikio wa wananchi umekuwa mkubwa ambapo zaidi ya wananchi 700 wamehudumiwa na wizara, huku hati zaidi ya 400 zikitolewa kwa wamiliki mbalimbali.

Aliwahimiza wananchi kutumia fursa ya maonesho hayo kufika katika banda la wizara kupata huduma mbalimbali za ardhi, ikiwemo ushauri wa kitaalamu, uthibitishaji wa umiliki wa viwanja, pamoja na kushughulikiwa changamoto zinazohusu ardhi na makazi.