Na John Bukuku – Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Kamati ya Utafiti wa Kuendeleza Wachimbaji Wadogo nchini Tanzania, Victor Tesha, amesema sekta ya madini inaendelea kuwa moja ya nguzo muhimu za mageuzi ya uchumi wa taifa kutokana na mchango wake katika ajira, mapato ya serikali, fedha za kigeni pamoja na kuchochea ukuaji wa sekta nyingine za kiuchumi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti ya kamati hiyo uliofanyika katika Hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam, Tesha alisema mchango wa sekta ya madini katika pato la taifa umeendelea kuongezeka kutoka asilimia 9.1 mwaka 2023 hadi zaidi ya asilimia 10 mwaka 2024 huku wastani wa asilimia 11.9 ukifikiwa kati ya Januari na Septemba 2025.
Alisema mafanikio hayo yametokana na maboresho ya sera, usimamizi mzuri wa sekta pamoja na uwekezaji uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Tesha alisema wachimbaji wadogo wana mchango mkubwa katika sekta hiyo kwani wanachangia takribani asilimia 40 ya mapato ya sekta ya madini, huku wakitoa ajira kwa maelfu ya Watanzania na kuimarisha biashara za ndani katika maeneo mbalimbali ya uchimbaji.
Hata hivyo alisema pamoja na umuhimu huo, wachimbaji wadogo bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa mitaji, taarifa za kijiolojia, matumizi ya teknolojia duni, mazingira hatarishi ya kazi pamoja na ukosefu wa mifumo rafiki ya kifedha.
Alieleza kuwa utafiti uliofanywa na kamati hiyo umebaini kuwa wachimbaji wengi bado wanategemea maarifa ya asili katika uchimbaji huku zaidi ya asilimia 72 wakiendelea kutumia njia za kawaida za uchenjuaji wa madini, hali inayosababisha uzalishaji mdogo na upotevu wa mapato.
Kwa mujibu wa Tesha, kamati hiyo imependekeza kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Madini Tanzania utakaosaidia kuongeza upatikanaji wa fedha, kugharamia tafiti za kijiolojia, kusaidia matumizi ya teknolojia bora pamoja na kuwaandaa wachimbaji wadogo kuwa na miradi inayoweza kukopesheka.
Alisema hatua hiyo ni muhimu kwani wachimbaji wengi wanaendesha shughuli zao kwa mtaji mdogo usiozidi shilingi milioni 10, jambo linalowazuia kuwekeza katika vifaa bora, wataalamu na upanuzi wa uzalishaji.
Aidha, Tesha alisema kamati imependekeza serikali kuimarisha mifumo ya mafunzo, usalama migodini, ulinzi wa mazingira pamoja na urasimishaji wa wachimbaji ili kuongeza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa taifa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA), John Bina, aliipongeza Serikali kwa kuendelea kusikiliza na kutekeleza mapendekezo yanayotolewa na wachimbaji wadogo nchini.
Bina alisema tofauti na ilivyokuwa zamani, kwa sasa wizara ya madini imekuwa karibu zaidi na wachimbaji jambo lililosaidia sekta hiyo kukua kwa kasi kubwa kupitia ushirikiano kati ya serikali na wadau wa madini.
Alisema changamoto kubwa inayowakabili wachimbaji wadogo ni upatikanaji wa mitaji na mikopo, hivyo akaiomba Serikali kuunga mkono mpango wa kuanzishwa kwa Benki ya Wachimbaji Tanzania ili kusaidia wachimbaji kupata fedha za kuendeleza shughuli zao.
Bina aliongeza kuwa utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa katika ripoti hiyo utafungua ukurasa mpya kwa wachimbaji wadogo nchini kwa kuongeza uzalishaji, ajira na kuwajengea uwezo wa kushindana katika soko la kimataifa la madini.

