Na John Bukuku – Dar es Salaam
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipanga kuifanya sekta ya madini kuwa injini kubwa ya ukuaji wa uchumi, uzalishaji wa ajira na kupunguza umasikini kupitia uwezeshaji wa wachimbaji wadogo nchini.
Profesa Mkumbo alisema hayo wakati akizindua rasmi Ripoti ya Mapendekezo ya Kuendeleza Wachimbaji Wadogo wa Madini katika hafla iliyofanyika Hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam, ambapo alieleza kuwa sekta ya madini ni moja ya sekta za kimkakati zilizopewa kipaumbele katika mipango ya maendeleo ya taifa.
Alisema serikali imefikia hatua hiyo baada ya kutambua kuwa pamoja na ukuaji mkubwa wa uchumi, bado kuna haja ya kuhakikisha wananchi wengi zaidi wananufaika moja kwa moja kupitia ajira, biashara na ushiriki wao katika shughuli za uzalishaji.
“Ukuaji wa uchumi lazima uendane na kupunguza umasikini na kuzalisha ajira. Hatuwezi kutegemea makampuni makubwa pekee kwa sababu yanatumia teknolojia kubwa inayohitaji watu wachache, lakini wachimbaji wadogo wana uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira kwa wananchi wengi,” alisema Profesa Mkumbo.
Aidha alisema hatua ya serikali kutenga asilimia 10 ya mapato ya sekta ya madini kwa ajili ya shughuli za utafiti ni uamuzi wa kihistoria utakaoleta mageuzi makubwa katika sekta hiyo kwa kuwa utaongeza upatikanaji wa taarifa sahihi za kijiolojia na kusaidia wachimbaji kufanya kazi kisasa zaidi.
Profesa Mkumbo alisema maamuzi yanayotokana na ushahidi wa kisayansi yana uwezo mkubwa wa kuleta mafanikio katika sekta mbalimbali, hivyo ripoti hiyo itakuwa nyenzo muhimu katika kufanya maamuzi sahihi kuhusu maendeleo ya wachimbaji wadogo nchini.
Aliipongeza Wizara ya Madini kwa kuandaa ripoti hiyo akisema imekuja wakati muafaka ambapo serikali inaendelea kusukuma agenda ya kuongeza ushiriki wa Watanzania katika uchumi wa madini na kuhakikisha rasilimali za taifa zinawanufaisha wananchi wengi zaidi.
Kwa upande wake Waziri wa Madini Anthony Mavunde alisema sekta ya madini imeendelea kufanya vizuri kwa kuvuka malengo ya ukusanyaji wa mapato yaliyowekwa na serikali.
Alisema hadi kufikia Juni 12, 2026, wizara hiyo ilikuwa imeingiza zaidi ya shilingi trilioni moja katika mfuko mkuu wa serikali ikiwa ni sehemu ya lengo la kukusanya trilioni 1.2 kwa mwaka wa fedha unaomalizika Juni 30, huku akibainisha kuwa mwaka uliopita sekta hiyo iliingiza trilioni 1.3.
Mavunde alisema mafanikio hayo yanathibitisha umuhimu mkubwa wa sekta ya madini katika uchumi wa taifa, huku akieleza kuwa wachimbaji wadogo wanachangia takribani asilimia 40 ya mapato yote ya sekta hiyo licha ya kukabiliwa na changamoto za mitaji, teknolojia na ukosefu wa taarifa sahihi za utafiti.
“Tunao wachimbaji wanaoshindwa kuongeza uzalishaji kwa kukosa vifaa vidogo kama pump na compressor. Hivyo ni wakati sasa wa serikali kuweka mfumo maalum wa kuwawezesha ili waongeze tija na mchango wao katika uchumi wa taifa,” alisema Mavunde.
Alisema serikali tayari imeanza kuchukua hatua mbalimbali za kuwawezesha wachimbaji hao ikiwemo kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania kupitia mfumo wa dhamana ya mikopo utakaowawezesha wachimbaji wadogo kupata mikopo hata pale wanapokosa dhamana zinazotakiwa na benki za biashara.
Kwa mujibu wa Mavunde, mfumo huo utaanza rasmi Julai Mosi mwaka huu kupitia taasisi ya Credit Guarantee Corporation ambayo itaanza na mtaji wa kati ya shilingi bilioni 300 hadi trilioni moja kwa ajili ya kusaidia sekta mbalimbali ikiwemo madini.
Waziri huyo alisema hatua nyingine inayochukuliwa ni kuendelea kuwapatia wachimbaji wadogo maeneo rasmi ya uchimbaji pamoja na kufuta leseni kwa wale wanaoshindwa kuendeleza maeneo yao kwa mujibu wa masharti ya leseni.
Alisema serikali pia imejipanga kuongeza uwekezaji katika tafiti za madini baada ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuridhia asilimia 10 ya mapato ya sekta hiyo kubaki kwa ajili ya shughuli za utafiti, hatua aliyoitaja kuwa ya kihistoria katika maendeleo ya sekta ya madini nchini.
Mavunde alisema dhamira ya serikali ni kuwasaidia wachimbaji wadogo kuondokana na uchimbaji wa kubahatisha na kuingia katika mfumo wa kisasa unaotumia teknolojia, tafiti na masoko rasmi ili kuongeza thamani ya madini na kukuza uchumi wa taifa.
Aliongeza kuwa serikali inalenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu kikubwa cha biashara ya madini barani Afrika kwa kuweka mazingira yatakayowawezesha wachimbaji kupata mitaji ya ndani na kuuza madini yao ndani ya nchi badala ya kutegemea masoko ya nje kama Dubai.
“Tunataka kuhamisha biashara ya dhahabu kutoka Dubai kuja Tanzania. Tukiwapa wachimbaji wetu mitaji na soko la uhakika, biashara yote ya madini itahamia Kahama, Geita na Chunya badala ya kutegemea wafadhili kutoka nje ya nchi,” alisema Mavunde.

