Na. Ssgt Mawazo Mtondo – Dodoma.

Mkuu wa Jeshi la Magereza, CGP Jeremiah Yoram Katungu, amewataka Maafisa Ustawi wa Jamii wa Jeshi la Magereza kuhakikisha wanawaelimisha wafungwa na mahabusu kuhusu haki na wajibu wao mara wanapopokelewa magerezani pamoja na taratibu zinazopaswa kufuatwa katika kipindi chote wanaposhikiliwa gerezani.

CGP Katungu ametoa maelekezo hayo leo Juni 12, 2026 wakati akifunga rasmi Mafunzo ya Maafisa Ustawi wa Jamii kuhusu Mwongozo wa Utekelezaji wa Programu za Urekebishaji yaliyofanyika kwa siku tatu katika Ukumbi wa Rugimbana, Msalato jijini Dodoma.

Amesema mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za Jeshi la Magereza za kuendelea kuboresha huduma za urekebishaji kwa wafungwa sambamba na kutekeleza maelekezo ya Serikali na mapendekezo ya Tume ya Kuboresha Vyombo vya Haki Jinai.

Akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo, CGP Katungu alisema mwongozo huo umebainisha maeneo muhimu yanayopaswa kuzingatiwa katika utekelezaji wa jukumu la urekebishaji, ikiwemo maadili ya kazi, dhana ya urekebishaji wa wafungwa, haki za binadamu katika utekelezaji wa programu za urekebishaji pamoja na matumizi sahihi ya nyaraka na fomu mbalimbali za kazi.

Aliwataka washiriki kutumia maarifa waliyojifunza kwa weledi na ufanisi ili kuleta mageuzi chanya katika utekelezaji wa jukumu la msingi la Jeshi la Magereza la kuwarekebisha wafungwa. Aidha, aliwahimiza kushirikiana na Wakuu wa Magereza kuanzisha na kuimarisha shughuli zinazolenga kuwapatia wafungwa elimu, maarifa na ujuzi wa kujitegemea.

Vilevile, aliwataka maafisa na askari wote wa Jeshi la Magereza kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia haki za wafungwa na mahabusu bila kuathiri usalama wao na wa magereza kwa ujumla. Alisisitiza umuhimu wa kudumisha upendo, mshikamano na umoja miongoni mwa watumishi wa Jeshi la Magereza ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu na kuendelea kulitumikia Taifa kwa ufanisi.

Awali akimkaribisha Mkuu wa Jeshi la Magereza, Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza, CP Nicodemus Tenga, alimshukuru kwa kuridhia kufanyika kwa mafunzo hayo yaliyolenga kuwajengea uwezo, maarifa na stadi za kiutendaji Maafisa Ustawi wa Jamii.

CP Tenga alisema mafunzo hayo pia yalitoa fursa kwa washiriki kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu mbalimbali za kuboresha utendaji wao katika maeneo ya kazi kwa lengo la kuimarisha huduma za urekebishaji ndani ya Jeshi la Magereza.