Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas James Lyimo amesema dawa za kulevya zinaendelea kuwa tishio kubwa kwa afya ya wananchi, ustawi wa familia, usalama wa jamii pamoja na maendeleo ya taifa kutokana na madhara yake ya kiafya, kijamii na kiuchumi.
Akizungumza leo Juni 12, 2026 katika uzinduzi wa filamu ya “Kifurushi” uliofanyika katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli jijini Dar es Salaam, Lyimo alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kudhibiti biashara na matumizi ya dawa za kulevya nchini.
Alisema hatua hizo zinajumuisha operesheni za ukamataji, utoaji wa tiba kwa waathirika wa dawa za kulevya pamoja na utoaji wa elimu kwa umma ili kujenga uelewa na ushiriki wa wananchi katika mapambano dhidi ya tatizo hilo.
“Kwa siku za hivi karibuni, Mamlaka imeendelea kubaini mbinu mbalimbali zinazotumiwa na wahalifu kusafirisha dawa za kulevya ikiwemo kupitia vyombo vya usafiri wa umma. Mara nyingi dawa hizo hufichwa kwenye mizigo na vifurushi vinavyoonekana kuwa vya kawaida,” alisema Lyimo.
Alieleza kuwa baadhi ya madereva, makondakta, wahudumu wa mabasi, wasafirishaji wa mizigo pamoja na abiria wamejikuta wakihusishwa na makosa ya dawa za kulevya baada ya kubeba mizigo au vifurushi wasivyovifahamu.
Kwa mujibu wa Lyimo, filamu hiyo imeandaliwa kuonesha uhalisia wa namna ambavyo mtu anaweza kuingia katika mtego wa kuwa sehemu ya wahalifu wa dawa za kulevya kwa kubeba mzigo au kifurushi asichokifahamu.
“Filamu hii inalenga kuongeza uelewa kwa madereva, makondakta, wahudumu wa mabasi, wasafirishaji wa mizigo, abiria na wananchi kwa ujumla kuhusu wajibu wao katika vita dhidi ya dawa za kulevya pamoja na madhara ya kijamii na kiuchumi yanayoweza kujitokeza kutokana na kitendo hicho,” alisema.
Aidha alisema DCEA ilifanya majadiliano na LATRA pamoja na Bodi ya Filamu Tanzania na kuona umuhimu wa kuandaa filamu hiyo kama moja ya njia za kutoa elimu kwa jamii ili kuzuia athari zinazoweza kusababishwa na usafirishaji wa dawa za kulevya.
Lyimo alisema kaulimbiu ya filamu hiyo ni “Usafiri Salama bila Dawa za Kulevya” na itaanza kuoneshwa katika mabasi yote yanayosafiri katika mikoa mbalimbali nchini.
Aliongeza kuwa Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli kimechaguliwa kwa uzinduzi huo kutokana na kuwa moja ya vituo vikubwa vinavyohudumia maelfu ya wasafiri kila siku hivyo kuwa sehemu sahihi ya kufikisha ujumbe huo kwa wakati mmoja kwa madereva, makondakta, wasafirishaji wa mizigo na abiria.
Kamishna Lyimo pia aliwataka wamiliki wa mabasi, makampuni ya usafirishaji na wadau wote wa sekta ya usafiri kuipa kipaumbele filamu hiyo kwa kuhakikisha inaoneshwa katika vyombo vyao vya usafiri ili kusaidia kutoa elimu na kuimarisha usalama wa jamii dhidi ya dawa za kulevya.
“Usikubali kubeba mzigo, kifurushi au bidhaa yoyote usiyoifahamu. Hakikisha unatambua unachobeba, kinatoka kwa nani na kinaelekea kwa nani. Kifurushi unachodhani ni cha kawaida kinaweza kubeba dawa za kulevya na kubadili maisha yako kwa matokeo hasi,” alisisitiza Lyimo.
Katika hatua nyingine, aliwashukuru wadau wote walioshiriki kufanikisha utengenezaji wa filamu hiyo akiwemo Bodi ya Filamu Tanzania, LATRA, wasanii, waandishi, waongozaji pamoja na wataalamu mbalimbali waliochangia kufikisha ujumbe huo kwa jamii kupitia sanaa.
“Kwa pamoja tunaweza kuzuia usafirishaji wa dawa za kulevya, kulinda vijana wetu, kuimarisha usalama wa jamii na kujenga Taifa lenye afya, nguvu kazi salama na maendeleo endelevu,” alisema.
Baada ya hotuba hiyo, Kamishna Jenerali huyo alizindua rasmi filamu ya “Kifurushi” na kuitangaza kuwa sehemu ya kampeni ya elimu kwa umma kuhusu madhara ya usafirishaji wa dawa za kulevya nchini.

