Na Silivia Amandius 

Kagera.

Shule ya Karume Day and Boarding Medium Primary School imefufua rasmi kituo chake cha ufundishaji wa michezo (Sports Academy) pamoja na kituo cha nguvu kazi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuibua vipaji vya vijana na kuwawezesha kujiajiri kupitia stadi mbalimbali.

Akizungumza baada ya kuwapokea wataalamu wawili wa michezo watakaosimamia programu hiyo, Mkurugenzi wa shule hiyo, Seif Mkude, amesema lengo kuu ni kuwapa vijana fursa ya kukuza vipaji vyao tangu wakiwa wadogo na kuwajengea msingi wa mafanikio katika maisha yao ya baadaye.

Mkude ametoa wito kwa wazazi na walezi mkoani Kagera kutumia fursa hiyo kwa kuwaruhusu watoto wao kushiriki katika mafunzo yatakayotolewa, akieleza kuwa michezo ni njia muhimu ya kukuza vipaji, nidhamu na ajira kwa vijana.

Amesema kabla ya kituo hicho kusitisha shughuli zake miaka iliyopita kutokana na changamoto mbalimbali, kilifanikiwa kuibua vipaji vya vijana wengi, baadhi yao wakifanikiwa kucheza katika ligi mbalimbali nchini na wengine kuendelea na soka katika nchi ya Hispania.

Kwa mujibu wa Mkude, shule hiyo imewaleta wataalamu wawili wenye uzoefu mkubwa katika michezo, ambao ni mshambuliaji wa zamani wa Young Africans S.C., Fumo Felician, pamoja na mwalimu wa soka Kessy Mziray, watakaokuwa na jukumu la kuwafundisha na kuwaendeleza vijana kuanzia umri wa miaka minane.