Na Mwandishi Wetu, Kilimanjaro
Ofisi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro imefanikiwa kusaidia kurejeshwa kwa pikipiki ya Ofisi ya Kijiji cha Kisangara, baada ya kubaini kuwa mali hiyo ilisajiliwa kwa jina binafsi la Mwenyekiti wa Kijiji hicho kinyume na malengo yaliyokusudiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 11, 2026, Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kilimanjaro, Sabas Salehe, alisema kuwa Mei 23, 2026 ofisi hiyo ilipokea taarifa kutoka kwa mtoa taarifa kuwa mwaka 2025 Mwenyekiti wa Kijiji cha Kisangara, Bw. Brayson Laurent Msofe, aliomba msaada wa kununuliwa pikipiki kwa ajili ya matumizi ya kijiji.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mwenyekiti huyo alieleza kuwa kulikuwa na umbali mrefu kutoka nyumbani kwake hadi Ofisi ya Kijiji pamoja na changamoto ya kuwafikia wananchi wanaoishi katika vitongoji mbalimbali, jambo lililokuwa likikwamisha utoaji wa huduma kwa ufanisi.
Salehe alisema kuwa baada ya maombi hayo kumfikia mtoa taarifa, Julai 15, 2025 alitoa fedha kiasi cha Sh milioni 2.8 ambazo ziliingizwa katika akaunti ya benki ya Kijiji cha Kisangara iliyopo NMB Mwanga kwa ajili ya kununua pikipiki mpya.
Hata hivyo, uchunguzi wa TAKUKURU ulibaini kuwa Mwenyekiti huyo alitumia fedha hizo kununua pikipiki mnamo Oktoba 17, 2025 lakini akaisajili kwa jina lake binafsi badala ya kijiji kama ilivyokuwa imekusudiwa.
“Kwa mujibu wa uchunguzi wa TAKUKURU, pikipiki hiyo ilisajiliwa kwa namba MC 266 FGQ na mmiliki kuonekana kuwa ni Bw. Brayson Laurent Msofe, jambo ambalo ni kinyume na malengo ya msaada huo,” alisema Salehe.
Alisema baada ya kufuatiliwa na TAKUKURU Mwanga, Mwenyekiti huyo alikiri kununua na kusajili pikipiki hiyo kwa jina lake na kueleza kuwa tayari alikuwa ameshaiuza.
Aidha, alisema baada ya mahojiano zaidi, Bw. Msofe alikubali kuwa alifanya makosa na kuahidi kurejesha mali hiyo ya kijiji.
Kutokana na hatua hiyo, Juni 8, 2026 Bw. Msofe akiwa ameambatana na wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji pamoja na Mtendaji wa Kijiji cha Kisangara walikwenda Moshi kwa ajili ya kununua pikipiki mpya ya kurejesha kwa matumizi ya kijiji.
Salehe alisema pikipiki hiyo mpya ilinunuliwa na kuhifadhiwa katika Ofisi za TAKUKURU Mkoa wa Kilimanjaro kabla ya kukabidhiwa rasmi leo kwa matumizi yaliyokusudiwa.
Katika hatua nyingine, TAKUKURU imetoa rai kwa viongozi wote waliopewa dhamana ya kusimamia mali za umma kuhakikisha mali hizo zinatumika kwa manufaa ya wananchi na si kwa maslahi binafsi.
“Ninatoa rai kwa viongozi wote waliopewa dhamana ya kulinda mali za umma kuhakikisha kuwa mali hizo zinatumika kwa maslahi ya umma na si vinginevyo, kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wametenda makosa ya rushwa,” alisema Salehe.
Kauli mbiu ya TAKUKURU inasema; “Kuzuia Rushwa ni Jukumu Lako na Langu; Tutimize Wajibu Wetu.” :::
