Na John Bukuku – Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, amesema kuwa ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini Urusi imeendelea kuionesha nafasi ya Tanzania katika ulingo wa diplomasia ya kimataifa duniani kupitia siasa, uchumi na biashara.
Akizungumza na waandishi wa habari Juni 7, 2026 jijini Dar es Salaam, Balozi Kombo amesema ziara hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha ushawishi wa Tanzania kimataifa, huku ikifungua fursa mpya za ushirikiano wa kiuchumi, kisiasa na kibiashara kati ya Tanzania na mataifa mbalimbali duniani.
Amesema ziara hiyo imeibua kile alichokiita mtikisiko chanya katika siasa za kimataifa, akibainisha kuwa hali hiyo inatokana na nafasi kubwa ya Urusi katika mahusiano ya kimataifa pamoja na ushirikiano wake na mataifa mengi yenye idadi kubwa ya watu duniani inayokadiriwa kufikia zaidi ya bilioni sita.
Aidha, Balozi Kombo amesema ushiriki wa Rais Samia katika majukwaa makubwa ya kimataifa unaendelea kuitangaza Tanzania kama taifa lenye mchango muhimu katika mijadala ya kimataifa kuhusu siasa, uchumi na biashara.
Pia ameongeza kuwa moja ya mafanikio yaliyojitokeza katika ziara hiyo ni kuendelea kuongezeka kwa matumizi ya lugha ya Kiswahili katika majukwaa ya kimataifa, jambo ambalo amesema linaongeza hadhi ya Tanzania na kuimarisha ushawishi wake wa kiutamaduni duniani.
Amebainisha kuwa matumizi ya Kiswahili katika ngazi za juu za uongozi wa kimataifa ni sehemu muhimu ya diplomasia ya utamaduni inayosaidia kuitangaza Tanzania na Afrika kwa ujumla katika jukwaa la dunia.
Vilevile, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha Kiswahili kinaendelea kukua na kuenea kimataifa, huku Tanzania ikiendelea kuwa mstari wa mbele katika kukienzi na kukiendeleza kama sehemu ya utambulisho na urithi wa taifa.

