Na Mwamvua Mwinyi, Chalinze
WATU wawili wamefariki dunia na magari mawili kuharibika vibaya kufuatia ajali ya kugongana uso kwa uso iliyotokea katika Daraja la Wami, Kata ya Mandela, Chalinze mkoani Pwani.
Ajali hiyo imetokea usiku kuamkia juni 7,2026 katika Barabara Kuu ya Dar es Salaam–Morogoro, ikihusisha gari lenye namba za usajili T.937 EHQ aina ya Toyota Hilux na gari lenye namba T.316 ENF/T.899 EQT aina ya Shacman.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, “Toyota Hilux ilikuwa ikiendeshwa na Juma Ridhiwani Juma kutoka Dar es Salaam kuelekea Tanga, huku gari la Shacman likiendeshwa na Innocent Beatus Salimu kutoka Tanga kuelekea Dar es Salaam.
Morcase ameeleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa Toyota Hilux aliyeshindwa kuchukua tahadhari na kujaribu kulipita gari lililokuwa limesimama mbele yake baada ya kupata hitilafu, na hivyo kwenda kugongana uso kwa uso na lori la Shacman.
Waliofariki katika ajali hiyo ni Hidaya Mgema Mzireni (51), mkazi wa Mtoni Kijichi, Dar es Salaam, aliyefariki papo hapo, pamoja na dereva wa Toyota Hilux, Juma Ridhiwani Juma (35), mkazi wa Dar es Salaam, aliyefariki dunia alipokuwa akipatiwa matibabu katika Kituo cha Afya cha Msata.
Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Msoga, Chalinze kwa taratibu zaidi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani amewakumbusha madereva wote kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani ili kuepusha ajali zinazotokana na uzembe.
Morcase ameongeza kuwa hatua kali za kisheria zitaendelea kuchukuliwa dhidi ya madereva watakaobainika kusababisha ajali kwa kutofuata sheria za usalama barabarani.
