Na Beda Msimbe, TBN, Petersburg
Rais Vladimir Putin wa Urusi amesema Tanzania ni lango kuu la kimkakati linalounganisha soko la Afrika Mashariki na masoko ya kimataifa.
Aidha, amesema kuwa katika kipindi ambacho uchumi wa dunia unaendelea kubadilika kuelekea mfumo wa nguzo nyingi za kiuchumi, Tanzania ina nafasi muhimu katika kufanikisha ustawi wa jamii mbalimbali duniani.
Akizungumza Juni 5, 2026 katika Jukwaa la Kimataifa la Uchumi la St. Petersburg, Rais Putin amesema Tanzania ni taifa la kimkakati katika ukanda wa Afrika Mashariki, akifananisha nafasi yake na ile ya Uzbekistan katika ukanda wa Asia ya Kati, ambapo mataifa hayo yanafanya kazi kama viungo muhimu kati ya uchumi wa kikanda na vituo vikuu vya biashara ya kimataifa duniani.
Kiongozi huyo alibainisha hayo alipokuwa akizungumzia mataifa ambayo, kutokana na nafasi zao za kijiografia na mahusiano ya kiuchumi, yanageuka kuwa madaraja muhimu kati ya kanda mbalimbali duniani.
Aliongeza kuwa mataifa yenye uwezo wa kuoanisha maendeleo yao ya ndani na miunganisho madhubuti kwenye vituo vipya vya ukuaji wa uchumi wa kimataifa yanazidi kuwa muhimu kadri mifumo ya biashara ya dunia inavyoendelea kubadilika.
Kauli hizi kutoka kwa Rais Putin zinakuja wakati Tanzania ikiendelea kupanua kwa kasi miundombinu yake ya usafirishaji, ikiwemo bandari na njia za biashara za kikanda, kwa lengo la kuimarisha nafasi yake kama kitovu kikuu cha biashara kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, hatua inayotafsiri kwa vitendo malengo ya ukuaji wa uchumi wa taifa.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alishiriki katika jukwaa hilo ambapo alipata nafasi ya kuelezea mambo mbalimbali yanayohusiana na uwekezaji na biashara.
Aidha, Rais Samia alisema Tanzania ipo tayari kushirikiana na mataifa yote, ikiwemo Urusi, katika kupeleka fursa mbalimbali za maendeleo kwa wananchi wake. Akijibu swali kuhusu vikwazo vinavyoikabili Urusi, Rais Samia alisema Tanzania haina vikwazo katika ushirikiano wake wa kimataifa, bali inafanya kazi na washirika wote wanaoitakia mema nchi yake.
