Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb)(Katikati), Mkurugenzi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania anayemaliza muda wake, aliyekuwa akiziwakilisha pia nchi za Malawi, Zambia na Zimbabwe, Bw. Nathan Belete (kushoto) na Mkurugenzi Mkazi Mpya wa Benki hiyo hapa nchini Bw. Firas Raad, wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa hafla ya kumuaga Bw. Belete na kumkaribisha Mkurugenzi Mpya Bw. Raad, hafla liyofanyika katika hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akizungumza wakati wa hafla ya kumuaga Mkurugenzi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania anayemaliza muda wake, aliyekuwa akiziwakilisha pia nchi za Malawi, Zambia na Zimbabwe, Bw. Nathan Belete (hayupo pichani) na kumkaribisha Mkurugenzi Mkazi Mpya wa Benki hiyo hapa nchini Bw. Firas Raad, hafla iliyofanyika katika hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam, ambapo alimshukuru Mkurugenzi huyo na Benki ya Dunia kwa mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi kupitia program na miradi mbalimbali.

Mkurugenzi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania anayemaliza muda wake, aliyekuwa akiziwakilisha pia nchi za Malawi, Zambia na Zimbabwe, Bw. Nathan Belete, akizungumza jambo wakati wa hafla ya kumuaga Mkurugenzi huyo iliyofanyika katika hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam, ambapo alisema kuwa Tanzania, katika miaka michache ijayo, itakuwa miongoni mwa nchi zilizopiga hatua kubwa kiuchumi na kijamii katika Bara la Afrika na duniani kwa ujumla kutokana na kujaaliwa kuwa na rasilimali nyingi.

Mkurugenzi Mkazi Mpya wa Benki ya Dunia nchini Bw. Firas Raad, akizungumza jambo wakati wa hafla ya kumuaga Mkurugenzi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania anayemaliza muda wake, aliyekuwa akiziwakilisha pia nchi za Malawi, Zambia na Zimbabwe, Bw. Nathan Belete (hayupo pichani), na kumkaribisha yeye, hafla iliyofanyika katika hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam, ambapo aliahidi kuendeleza pale alipoishia mtangulizi wake na kuimarisha zaidi  uhusiano na ushirikiano kati ya Benki na Tanzania.

Baadhi ya Wadau mbalimbali wa sekta ya fedha  na watumishi wa Benki ya Dunia nchini, wakisikilizia hotuba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (hayupo pichani) akizungumza wakati wa hafla ya kumuaga Mkurugenzi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania anayemaliza muda wake, aliyekuwa akiziwakilisha pia nchi za Malawi, Zambia na Zimbabwe, Bw. Nathan Belete (hayupo pichani), na kumkaribisha Mkurugenzi Mkazi wa Benki hiyo, Bw. Firas Raad, hafla iliyofanyika katika hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Fedha Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (Katikati), Mkurugenzi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania anayemaliza muda wake, aliyekuwa akiziwakilisha pia nchi za Malawi, Zambia na Zimbabwe, Bw. Nathan Belete (wa pili kushoto mstari wa nyuma) na Mkurugenzi Mkazi Mpya wa Benki hiyo hapa nchini Bw. Firas Raad (wa nne kulia), wakiwa katika picha ya pamoja na wadau mbalimbali kutoka sekta binafsi waliohudhuria katika hafla ya kumuaga Bw. Belete na na kumkaribisha Mkurugenzi Mpya, Bw. Raad,  hafla iliyofanyika katika hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,WF, Dar es Salaam)

Na Benny Mwaipaja, Dar Es Salaam

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) amesema kuwa Benki ya Dunia ina mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi kupitia program na miradi mbalimbali ya kimkakati inayotekelezwa nchini kupitia misaada na mikopo nafuu inayotolewa na Taasisi hiyo kubwa ya fedha duniani.

Mhe. Balozi Omar alisema hayo jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla ya kumuaga aliyekuwa Mkurugenzi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania, aliyekuwa akiziwakilisha pia nchi za Malawi, Zambia na Zimbabwe, Bw. Nathan Belete na kumkaribisha Mkurugenzi Mkazi Mpya wa Benki hiyo hapa nchini Bw. Firas Raad,

Akizungumza kwenye tukio hilo lililoandaliwa na Benki ya Dunia kama Mgeni Rasmi, Mhe. Balozi Omar alimpongeza Bw. Belete kwa uongozi wake makini na kuisaidia nchi kuvuka salama misukosuko ya kiuchumi iliyosababishwa na majanga mbalimbali ukiwemo ugonjwa wa UVIKO 19, mizozo ya kisiasa, kuongezeka kwa gharama za mikopo na mabadiliko ya tabianchi.

“Benki ya Dunia chini ya uongozi wake imeiwezesha nchi kutekeleza miradi yake ya kipaumbele katika sekta za usafiri, nishati, maji, elimu, afya, maendeleo ya mijini, ulinzi wa jamii,  kustahimili mabadiliko ya tabianchi iliyosaidia kuboresha maisha ya mamilioni ya Watanzania,” alisema Mhe. Balozi Omar, akimshukuru Mhe. Belete kwa kujitolea kwake, ushirikiano na ushiriki wake wa  karibu na taasisi za Serikali na wadau wengine.

Aidha, Mhe, Balozi Omar, alimkaribisha rasmi Mkurugenzi Mkazi mpya wa Benki ya Dunia, Bw. Firas Raad, ambaye sasa atasimamia shughuli za Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania Malawi,  Zambia na Zimbabwe.

Mhe. Balozi Omar alisema kuwa Bw. Raad anakuja Tanzania wakati muhimu kwani nchi, chini ya Uongozi mahiri  wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaendelea kutekeleza malengo ya muda mrefu ya maendeleo chini ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 (Dira2050) pamoja na mageuzi yanayoendelea ya kuimarisha ushindani, taasisi na kuvutia uwekezaji.

Alitoa wito kwa Benki ya Dunia pamoja na Shirika lake linalosaidia Sekta Binafsi (IFC) kuendeleza ushirikiano thabiti na Tanzania ili kukusanya mitaji, kuchochea uwekezaji wa sekta binafsi, kuboresha ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi na kuunga mkono miradi ya mabadiliko katika miundombinu, nishati, dijitali, kilimo, elimu, afya na kustahimili mabadiliko ya tabianchi.

“Serikali ya Tanzania iko tayari kufanya kazi kwa karibu na Benki ya Dunia ili kuharakisha mabadiliko ya kiuchumi, kuimarisha ustahimilivu, kukuza ustawi na kutengeneza fursa kwa vizazi vijavyo kiuchumi na kijamii,” alisema Mhe. Balozi Omar, akiahidi ushirikiano kamili kwa Bw. Raad.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam, Bw. Nathan Belete alieleza kuwa anaondoka nchini baada ya kupangiwa majukumu mengine na Taasisi yake akiwa na moyo wa furaha na shukrani kutokana na maendeleo makubwa ambayo nchi imepiga kiuchumi na kijamii.

Alisisitiza kuwa Tanzania, katika miaka ya hivi karibuni, itakuwa miongoni mwa nchi zilizopiga hatua kubwa kiuchumi na kijamii katika Bara la Afrika na duniani kwa ujumla kutokana na kujaaliwa kuwa na rasilimali lukuki ambazo zikiendelezwa ipasavyo, zitakuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi na watu wake.

Alisema kuwa Tanzania imejaaliwa kuwa na kila aina ya rasilimali, yakiwemo madini ya kila aina, kilimo, maziwa, bahari pamoja na utajiri mkubwa wa srkta ya maliasili na utalii ambavyo vinaweza kubadili uchumi wa nchi kwa kushirikiana na sekta binafsi.

Naye Mwakilishi Mkazi Mpya wa Benki ya Dunia, Bw. Firas Raad, aliahidi kuendeleza pale alipoishia mtangulizi wake na kwamba atahakikisha uhusiano na ushirikiano kati ya Benki ya Dunia na Tanzania unakuwa imara zaidi.

Hafla hiyo iliyohudhuriwa na Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini, Wakuu wa Mashirika mbalimbali ya Kimataifa yanayofanya shughuli zake hapa nchini pamoja na wadau wengine kutoka Taasisi za Umma na Sekta binafsi, ilihitimishwa kwa kunyanyua glasi kusherehekea mchango wa Bw. Nathan Belete na kumtakia mafanikio endelevu, pamoja na kumkaribisha  Bw. Raad katika wadhifa wake mpya, na kuenzi uhusiano wa kimkakati kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Benki ya Dunia.