Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
Juni 4, 2026
Madereva wanane wamefungiwa leseni huku wengine 55 wakifikishwa mahakamani kwa makosa mbalimbali ya usalama barabarani kufuatia operesheni zilizofanywa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani ndani ya mwezi Mei 2026.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, alisema jumla ya makosa 16,833 ya usalama barabarani yalibainika katika kipindi hicho.
Alifafanua wahusika walichukuliwa hatua za kisheria na kupewa elimu kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria za usalama barabarani.
Morcase alieleza katika operesheni nyingine, jeshi hilo liwakamata watuhumiwa 11 wa wizi wa mifugo na kufanikiwa kuokoa ng’ombe 28 waliokuwa wameibwa katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Aliongeza kuwa kesi 298 zilifikishwa mahakamani ndani ya kipindi hicho, huku kesi 128 zikisikilizwa na kukamilika.
Kwa mujibu wa Morcase, baadhi ya watuhumiwa walihukumiwa vifungo vya miaka 30, miaka 37 na kifungo cha maisha kwa makosa mbalimbali yakiwemo ubakaji, kujeruhi na ulawiti.
Kadhalika aliwahimiza wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu, kuwafichua wahalifu na kufika vituo vya polisi kutambua mali zilizookolewa ili kuthibitisha umiliki wake.
Jeshi hilo linaendelea kutoa elimu kwa wananchi kupitia mikutano ya hadhara, vyombo vya habari, shule na taasisi mbalimbali kwa lengo la kuimarisha usalama wa wananchi na mali zao.
