Na. OWM (KAM) Dodoma
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Dkt. Evaline Munisi amekutana na kufanya kikao kazi na Wakurugenzi pamoja na wataalamu wa Idara ya Ajira na Ukuzaji Ujuzi kutoka Ofisi hiyo kwa lengo la kuimarisha utekelezaji wa majukumu, kuongeza ufanisi wa kazi na kuimarisha ushirikiano katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Katika kikao hicho kilichofanyika ofisini kwake Dodoma Juni 04,2026 , Dkt. Munisi ameitaka idara hiyo kuongeza juhudi katika kutangaza fursa mbalimbali za ajira na programu za ukuzaji ujuzi zinazotolewa na Serikali ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi na kuwawezesha kunufaika na fursa hizo kwa wakati.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa ubunifu, uwajibikaji na ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu ya idara hiyo ili kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakuwa na tija, zinawafikia walengwa ipasavyo na kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.
Dkt. Munisi ameelekeza idara hiyo kuweka mkazo katika uboreshaji wa takwimu za soko la ajira na kufanya tathmini ya mara kwa mara ya mahitaji ya ujuzi katika sekta mbalimbali. Alisema hatua hiyo itawezesha Serikali kuandaa programu zinazoendana na mahitaji halisi ya waajiri na soko la ajira kwa ujumla.
Kwa upande wao, Wakurugenzi wa Idara hizo Bi.Alana Nchimbi na Bi.Jane Sorogo wamemshukuru Naibu Waziri kwa maelekezo na mwongozo alioutoa ambapo wameahidi kuongeza kasi ya utekelezaji wa mipango ya idara, ikiwemo kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi, vyuo vya ufundi na taasisi za elimu ya juu ili kuhakikisha vijana wanapata ujuzi unaohitajika sokoni.
Kikao hicho ni sehemu ya jitihada endelevu za Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano kuhakikisha kuwa Sera ya Taifa ya Ajira ya mwaka 2008 inatekelezwa kwa vitendo, changamoto za ajira zinapungua na fursa za kiuchumi zinapanuliwa kwa vijana na makundi mengine katika jamii.
