NA DENIS MLOWE IRINGA
MSAJILI wa Bodi ya Maziwa Tanzania, Profesa George Msalya, ametoa wito kwa wanahabari nchini kutumia kalamu na majukwaa yao kuisaidia jamii kupata uelewa mpana kuhusu umuhimu wa maziwa na mchango wake katika uchumi wa taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Royal Palm mjini Iringa, wakati wa mafunzo kwa wanahabari kuelekea maadhimisho ya Wiki ya Maziwa, Profesa Msalya alisema kuwa sekta ya habari ina nafasi muhimu katika kuifikisha elimu sahihi kwa wananchi, hususan katika maeneo ambayo viongozi hawawezi kuyafikia kwa wakati mmoja.
Alisema kwa miaka mitatu mfululizo Bodi ya Maziwa imekuwa ikikutana na wanahabari ili kuhakikisha ujumbe unaohusu uzalishaji wa maziwa, afya ya maziwa, usalama wa bidhaa za maziwa na fursa za uwekezaji unawafikia Watanzania kwa usahihi.
Profesa Msalya alibainisha kuwa wanahabari ni daraja kati ya wataalamu, serikali na wananchi, na kwamba kupitia kazi zao wana uwezo wa kubadilisha maisha ya Watanzania kwa kutoa taarifa zinazowawezesha kufanya maamuzi sahihi katika uzalishaji wa mifugo, maziwa na masuala ya lishe.
Ameongeza kuwa maziwa ni uchumi, ni lishe na ni ajira, hivyo kunahitajika ushirikiano wa muda mrefu kati ya Bodi ya Maziwa na vyombo vya habari ili kuhakikisha elimu sahihi inawafikia wananchi katika maeneo yote ya nchi.
Alimalizia kwa kuwataka wanahabari kuendelea kutumia ujuzi na nguvu walizo nazo kuisaidia Tanzania kupata mabadiliko chanya katika sekta ya maziwa na ufugaji kwa ujumla.
