Na Hassan Kimweri, WAF – Dar es Salaam

Kuelekea utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa na Waziri wa Afya Tanzania Bara Mhe. Mohamed Mchengerwa pamoja na Waziri wa Afya wa Jamhuri ya watu China Mhe. Haichao Lei yaliyofikiwa kati ya nchi hizo mbili kwenye kikao kilichofanyika pembezoni mwa kikao cha 79 cha Shirika la Afya Duniani (WHA) ikiwa ni juhudi za Serikali katika kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya.

Maazimio hayo ni pamoja na kuimarisha huduma za Afya hususan katika kukabiliana na magonjwa ya milipuko, kutanua huduma za matibabu ya moyo kwa watoto na kuboresha huduma za tiba asili na tiba mbadala.

Kufuatia maazimio hayo, Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe leo Mei 28, 2026 amekutana na ujumbe wa Wizara ya Afya kutoka China katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya jijini Dar es Salaam na kujadiliana mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya afya ili kuongeza uwezo wa nchi kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiafya ikiwemo magonjwa ya milipuko na yale yanayohitaji ubingwa bobezi.

“Katika kikao hiki tumejadili maeneo mbalimbali ya ushirikiano ikiwemo kuimarisha huduma za Tiba Asili na Tiba Mbadala, kuendeleza afua za kukabiliana na magonjwa yanayoathiri afya ya jamii hususan katika mikoa iliyopo katika hatari zaidi ya kupata maambukizi pamoja na kuongeza uwezo wa wataalamu wa afya kupitia mafunzo katika vyuo vya nchini China,” amesema Dkt. Magembe

Aidha, Dkt. Magembe amesema Serikali ya Tanzania inalenga kuipanua Hospitali ya Jakaya Kikwete ili iwe kituo cha umahiri barani Afrika katika kutoa huduma bobezi za moyo, hatua itakayosaidia kuongeza upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi wa Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Kwa upande wake, Kiongozi wa ujumbe huo kutoka China, Dkt. Gu Zhiqiang ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa kutoka Wizara ya Afya ya China amesema Serikali ya China ipo tayari kuendelea kushirikiana na Tanzania kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya afya kulingana na vipaumbele vya Tanzania.

Pia, Dkt. Gu amepongeza maendeleo ya Hospitali ya Jakaya Kikwete akisema hospitali hiyo imeonyesha mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka kumi kwa kutoa huduma bobezi kwa wananchi wa Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.

Kikao hiki kinaenda sambamba na ziara ya kutembelea mikoa kadhaa nchini, Taasisi ya Moyo JKCI, Hospitali ya Taifa Muhimbili, Kituo cha Utafiti wa magonjwa ya binadamu NIMR na Chuo Kikuu cha Sayansi za Tiba MUHAS.