Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa kushirikiana na Shirika la Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo (EMEDO) wametangaza rasmi kuanzishwa kwa Tuzo za Waandishi wa Habari zinazolenga kuhamasisha elimu kuhusu hali ya hewa, tahadhari za mapema na usalama majini nchini.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Mbezi Garden jijini Dar es Salaam, Afisa Uchechemuzi kutoka EMEDO, Bi. Mary Francis Mahemba alisema vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kuelimisha jamii kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi, majanga yanayosababishwa na hali mbaya ya hewa pamoja na hatua za kujikinga.

Alisema kupitia tuzo hizo, waandishi wa habari watatambuliwa kwa mchango wao katika kusambaza taarifa sahihi zinazosaidia kuokoa maisha ya wananchi na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu usalama majini.

“Waandishi wa habari ni wadau muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu tahadhari za hali ya hewa, usalama majini na hatua za kujikinga dhidi ya majanga. Kupitia tuzo hizi tunatambua mchango wao katika kujenga jamii salama na inayotambua hatari za kuzama maji,” alisema Bi. Mahemba.

Kwa mujibu wa waandaaji, tuzo hizo zinalenga kuhamasisha utayarishaji wa habari zenye ubora kuhusu matukio ya hali mbaya ya hewa na athari zake kwa jamii, tahadhari za mapema za hali ya hewa, usalama wa vyombo vya usafiri majini, uzuiaji wa ajali na vifo vitokanavyo na kuzama maji pamoja na ustahimilivu wa jamii dhidi ya majanga yanayohusiana na hali ya hewa.

Tuzo hizo zitawahusisha waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya redio, televisheni, magazeti, mitandao ya kijamii na majukwaa ya kidijitali nchini Tanzania.

Waandishi wamealikwa kuwasilisha kazi zao zilizochapishwa au kurushwa hewani ndani ya kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Agosti 1, 2025 hadi Agosti 30, 2026 kupitia barua pepe za [email protected] au [email protected].

Kwa upande wake, Meneja Masoko na Uhusiano wa TMA, Bi. Monica Mutoni alisema matumizi ya taarifa za hali ya hewa na mifumo ya tahadhari za mapema yana mchango mkubwa katika kuokoa maisha ya wananchi hususan wale wanaotegemea shughuli za maji ikiwemo uvuvi na usafiri wa majini.

Bi. Mutoni alisema TMA itaendelea kushirikisha wadau mbalimbali ili kuongeza thamani ya Tuzo za Wanahabari wa Masuala ya Hali ya Hewa nchini na kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za umma, mashirika ya kiraia pamoja na vyombo vya habari.

Aliongeza kuwa ushirikiano huo ni sehemu ya juhudi za kuendelea kuimarisha uelewa wa jamii, usambazaji wa taarifa sahihi za hali ya hewa na matumizi yake katika shughuli za kiuchumi na kijamii.