Na. Hance Mbena – Serengeti
Katika muendelezo wa kuitangaza Tanzania duniani kupitia utalii wa michezo, leo Mei 28, 2026, bingwa wa masumbwi duniani, Terence “Bud” Crawford, amekabidhiwa rasmi ubalozi wa utalii baada ya kukutana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji. Tukio hilo limefanyika ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ikiwa ni siku ya tano ya ziara yake nchini.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Dkt. Kijaji alieleza kuwa Serikali ya Tanzania chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeendelea kuifungua na kuitangaza sekta ya utalii kimataifa kupitia kampeni mbalimbali za kuitangaza nchi, ikiwemo filamu za “Tanzania: The Royal Tour” na “Amazing Tanzania” ambazo zimeendelea kuvutia wageni na watu mashuhuri kutoka mataifa mbalimbali duniani kutembelea Tanzania.
“Michezo ni sehemu muhimu ya ajira na maendeleo ya uchumi, lakini pia imekuwa daraja la kuunganisha Tanzania na watu mashuhuri duniani. Kupitia michezo tunaendelea kuitangaza Tanzania kimataifa na kufungua fursa mpya za utalii, uwekezaji na ajira kwa vijana,” amesema Waziri Kijaji.
Aidha, Waziri Kijaji alisisitiza kuwa Serikali inatarajia kuendelea kupokea watu mashuhuri kutoka mataifa tofauti duniani watakaotembelea vivutio vya utalii nchini, hatua ambayo itaendelea kuongeza thamani ya utalii wa Tanzania katika soko la kimataifa. Fauka ya hayo Waziri Kijaji amemkabidhi cheti cha kutambua mchango wake na kumpa ubalozi wa kuvitangaza vivutio vya utalii vinavyopatikana nchini kwa mwanamasumbwi huyo.
Kwa upande wake, mwanamasumbwi Crawford amepongeza ukarimu wa Watanzania pamoja na uzuri wa vivutio vya asili alivyovitembelea katika Hifadhi za Taifa Tarangire na Serengeti tangu kuwasili kwake nchini Mei 24, 2026, huku akiahidi kwenda kuwa balozi mzuri wa vivutio vya utalii Tanzania.
Naye, Kamishna wa Uhifadhi, CPA Musa Nassoro Kuji alieleza kuwa utalii wa michezo unaviongezea sifa na kuvitangaza vivutio vinavyopatikana nchini, pia amesisitiza kuendelea na zao hili la utalii wa michezo ambalo litachangia kufungua utalii wa Tanzania duniani, hivyo kuchangia kuongeza pato la Taifa.
Akiwa ndani ya Hifadhi ya Serengeti, bingwa huyo wa masumbwi atashiriki katika shughuli mbalimbali za kitalii zitakazosaidia kuitangaza hifadhi hiyo. Shughuli hizo ni pamoja na utalii wa puto (balloon safari), utalii wa kutumia gari (game drive), pamoja na utalii wa gari nyakati za usiku (night game drive) utakao mpa fursa ya kushuhudia maisha ya wanyamapori katika mazingira yao halisi wakati wa usiku.
Hifadhi za Taifa zimeendelea kuwa sumaku ya kuwavutia watu mashuhuri, wakiongozwa na bondia nguli Terence “Bud” Crawford pamoja na nyota wa zamani wa soka wa klabu ya Manchester United na timu ya taifa ya Uingereza, Rio Ferdinand. Ujio wa magwiji hawa ni kielelezo tosha cha mafanikio ya mkakati wa Serikali, kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, katika kuunganisha utalii na michezo kuitangaza Tanzania.

