Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Bungeni Dodoma

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Deogratius Akwilapo amesema kuwa Wizara yake itaendelea kuimarisha uratibu na usimamizi wa maendeleo ya sekta ya ardhi kwa kuzingatia vipaumbele vilivyoainishwa katika mwaka wa fedha 2026/2027.Amebainisha kuwa vipaumbele hivyo vinahusisha kuongeza kasi ya upangaji, upimaji na umilikishaji wa ardhi pamoja na kuimarisha matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Dkt. Akwilapo ameyasema hayo leo Mei 28, 2026 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Amesema kuwa Wizara pia itaendelea kutatua migogoro ya ardhi, kupima mipaka ya vijiji, kuimarisha mabaraza ya ardhi na nyumba ya wilaya pamoja na kuendeleza makazi na miji ya kisasa nchini.Aidha, ameongeza kuwa Serikali itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo Programu ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi, Mradi wa Uimarishaji wa Miundombinu ya Upimaji na Ramani pamoja na uendelezaji wa maeneo chakavu mijini.

Pia amebainisha kuwa Wizara itaendelea kuimarisha usimamizi wa sekta ya milki, kuongeza uwekezaji katika sekta ya nyumba pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya umiliki wa ardhi.