Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Paul Makonda, amesema Serikali inafikiria kuzifanya Mbio za Siku ya Afrika kuwa za Kimataifa ili kufanikisha lengo la kuleta Maendeleo ya pamoja kwa bara la Afrika.
Akizungumza wakati wa hafla ya kufunga mbio hizo Mhe. Makonda alisema mbio za Siku ya Afrika si mbio za kawaida bali ni ishara ya ushindi wa Waafrika dhidi ya ukoloni pamoja na jitihada zao za kuendelea kupigania uhuru, amani na ustawi wa bara hilo.
Akiongelea kuhusu mshikamano na uwajibikaji, Mhe. Makonda alisema hakuna taifa jingine litakalokuja kuijenga au kuilinda Tanzania au Afrika isipokuwa Watanzania au Waafrika wenyewe.
“Hakuna mtu atakayekuja kulinda nchi kwa ajili yetu. Ni jukumu letu sisi wenyewe watanzania na waafrika kwa ujumla kufanya kazi na kuhakikisha tunalinda na kuendeleza nchi yetu na bara letu,” alisisitiza.
Aliongeza kuwa Waafrika wanapaswa kushirikiana kutatua changamoto zao kwa kutumia nguvu, umoja na rasilimali walizonazo.
“Sisi ni Waafrika, na tunapaswa kufanya kazi pamoja na kutatua matatizo yetu sisi wenyewe,” alisema na kuwasihi Watanzania na Waafrika kwa ujumla kutumia kipindi hiki kama fursa ya kuimarisha mshikamano kulinda mustakabali wa bara la Afrika.
Waziri Makonda alitoa rai kwa Watanzania na Waafrika kwa ujumla kufanya kazi pamoja ili kulinda na kuendeleza bara lao, akisisitiza kuwa hakuna mtu mwingine atakayekuja kuijenga au kuilinda Afrika isipokuwa Waafrika wenyewe.
Alihimiza jamii kushirikiana kutatua changamoto zao na kuhakikisha nchi pamoja na jamii zao zinakuwa sehemu salama za kuishi kwa amani, mshikamano na maendeleo endelevu.

