Na Oscar Assenga,TANGA

Wazazi, walezi na waajiri nchini wamehimizwa kuhakikisha watoto wanawakatia bima ya afya mapema ili kuwaepusha na changamoto za gharama kubwa za matibabu na kuwawezesha kupata huduma za afya kwa wakati wanapougua.

Wito huo umetolewa leo na Afisa Matekelezo wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Tanga, Macrina Clemens, wakati wa utoaji wa elimu kuhusu bima ya afya ulioambatana na zoezi la upimaji wa afya na usajili wa wanachama wa vifurushi mbalimbali katika Kanisa la KKKT Ushirika wa Makorora, jijini Tanga.

Akizungumza na waumini wa kanisa hilo, Macrina alisema afya ni mtaji muhimu kwa maendeleo ya familia na Taifa, hivyo kujiunga na bima ya afya ni uwekezaji unaowalinda wananchi dhidi ya gharama zisizotarajiwa za matibabu.

Alisema wazazi wanaowakatia watoto wao bima ya afya hupata uhakika wa matibabu wakati wowote mtoto anapougua, jambo linalowapa utulivu wa akili na kuwawezesha watoto kuendelea na masomo bila kukatishwa na changamoto za kifedha.

“Mzazi anapokuwa na bima ya afya kwa mtoto wake anakuwa na uhakika wa kupata matibabu kwa wakati, hivyo kuepuka usumbufu wa kutafuta fedha za dharura kila ugonjwa unapojitokeza,” alisema.

Macrina alisema wanafunzi wanaosoma katika shule mbalimbali wanaweza kujiunga na bima ya afya kupitia shule zao kwa gharama ya Sh50,400 kwa mwaka mzima wa masomo, huku watoto ambao bado hawajaanza shule wakijiunga kupitia vifurushi mbalimbali vinavyotolewa na NHIF.

Alisema Serikali inaendelea kutekeleza azma ya kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa na bima ya afya, hivyo akazitaka taasisi za elimu, wazazi, walezi, waajiri na wamiliki wa kampuni binafsi kutumia fursa hiyo kuwaandikisha watoto na wafanyakazi wao.

“Bima ya afya si gharama, ni kinga ya maisha. Ukiwa na bima unakuwa na uhakika wa kupata daktari, dawa na huduma za matibabu bila kubeba mzigo mkubwa wa kifedha pale unapougua,” alisema.

NHIF imeendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya wananchi kuhusu umuhimu wa bima ya afya ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuongeza idadi ya Watanzania wanaonufaika na huduma hiyo na kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya nchini.