Na Mwandishi Wetu, Handeni
Mahakama ya Wilaya ya Handeni mkoani Tanga imemtia hatiani mwalimu mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kosa la wizi akiwa mtumishi wa umma, kufuatia ubadhirifu wa fedha za mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni.
Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu wa Wilaya, Stephano Mkoye Kushaba, katika kesi ya jinai namba 7073/2026, ambapo mshtakiwa alikutwa na hatia ya kosa la wizi akiwa mtumishi wa umma kinyume na vifungu vya 258(1)(2)(a), 265 na 270 vya Kanuni za Adhabu, Sura ya 16, Marejeo ya mwaka 2022.
Baada ya kutiwa hatiani, mahakama ilimhukumu kifungo cha nje cha mwaka mmoja na kumuamuru kurejesha kiasi cha shilingi 430,000, ikiwa ni sehemu ya fedha alizofanyia ubadhirifu.
Ilidaiwa mahakamani kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo katika nyakati tofauti alipokuwa akitekeleza jukumu la kukusanya mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni kwa kutumia mashine ya POS.
Katika kipindi hicho, alikusanya jumla ya shilingi 2,616,950 kutoka kwa wananchi, lakini badala ya kuziwasilisha benki kwenye akaunti ya Halmashauri, alizitumia kwa manufaa yake binafsi.
Hukumu hiyo ilitolewa mbele ya mwendesha mashtaka wa TAKUKURU, Reuben Ngassa, baada ya mshtakiwa kufikia makubaliano ya kukiri kosa katika Ofisi ya Mashtaka, hatua iliyowezesha shauri hilo kuhitimishwa kwa njia ya makubaliano.
