Mabigwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara Yanga Sc imeibuka na ushindi wa mabao 3-0 ya dhidi ya Singida Black Stars katika mchezo uliochezwa leo Ijumaa Mei 22, 2026 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, na kufikisha pointi 57 huku Simba ikiwa nafasi ya pili na pointi 55.

Katika mchezo huo kiungo mshambuliaji wa Yanga, Allan Okello, ameendelea kuonyesha umwamba wake kufuatia kufunga katika mchezo wa nne mfululizo wa Ligi Kuu Bara wakati timu hiyo ikirejea kileleni mwa msimamo baada ya jana kushushwa na Simba.

Okello aliwapa raha mashabiki wa Yanga dakika ya 13 ya mchezo huo, ikiwa ni rekodi kwa timu hiyo ya Wananchi ikiwa ni mchezaji pekee aliyefungua akaunti ya mabao katika mechi nne mfululizo.

Yanga ambayo ilikuwa ikisaka ushindi wake wa kwanza kufuatia kufungwa katika mechi ya mwisho ya ligi, ilionekana kuwa na nguvu kubwa kwenye safu yake ya ushambuliaji.

Baada ya Singida BS kuruhusu bao hilo la mapema, kocha wa kikosi hicho, Muhibu Kanu alifanya mabadiliko ya kwanza ambayo yalizua gumzo.

Katika dakika ya 23, alimtoa kipa Metacha Mnata ambaye hakuonekana kukubaliana na mabadiliko hayo na kuingia Amas Abasogie, ilibidi wachezaji wenzake kuongea naye kabla ya kutoka.

Katika dakika ya 62, Yanga ilifanya mabadiliko mengine kwa kumtoa Prince Dube na kuingia Depu. Wakati ambao Singida BS ikitafuta bao kurejea mchezoni, Okello alipiga msumari wa tatu.

Mabao hayo yamemfanya Okello kuwa na idadi sawa ya mabao na Prince Dube wote wakiwa na tisa, licha ya kutua Jangwani wakati wa dirisha dogo la Januari 2026, mbali na idadi hiyo ya mabao pia ametoa asisti saba.