Na Hassan Kimweri, WAF – Dodoma 

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya anayeshughulikia Dawa na Vifaa Tiba, Bw. Emmanuel Tayari, amewataka Viongozi wa huduma za afya nchini hususani Wauguzi na Wakunga kuleta mabadiliko ya kweli kwa kutoa huduma zinazozingatia utu wa mgonjwa, uwajibikaji na matumizi ya teknolojia katika kuboresha huduma.

Bw. Tayari amesema hayo leo Mei 22, 2026 wakati akifunga mkutano mkuu wa mwaka wa wauguzi viongozi uliojadili namna ya kuimarisha huduma za afya nchini kupitia uongozi wenye maono, nidhamu ya kazi na usimamizi bora wa huduma kwa wananchi.

“Sekta ya afya ipo katika hatua muhimu ya mageuzi makubwa yanayolenga kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika, kuboresha afya ya mama na mtoto pamoja na kuimarisha matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma za afya katika ngazi zote,” amesema Bw. Tayari

Aidha, Bw. Tayari amesisitiza kuwa mageuzi hayo hayawezi kufanikiwa bila kuwa na viongozi wa uuguzi na ukunga wenye uwezo wa kusimamia maadili, ubora wa huduma na kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma zenye heshima na huruma.

Katika mkutano huo pia imeelezwa kuwa hakuna mageuzi ya kweli katika sekta ya afya bila ushiriki mkubwa wa wauguzi na wakunga ambao ndio wanaobeba jukumu la msingi katika utoaji wa huduma kwa wananchi kuanzia Zahanati hadi Hospitali za Rufaa.

Pamoja na mafanikio yaliyopatikana, Bw. Tayari amesema bado kuna changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa watumishi, mzigo mkubwa wa kazi, pamoja na uhitaji wa mafunzo endelevu kwa wataalamu wa afya kwa kuwa sekta ya afya ikikua changamoto zinaongezeka. 

Hata hivyo, Bw. Tayari amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na changamoto hizo kupitia ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya afya, kuimarisha mazingira ya kazi, kuongeza bajeti ya sekta ya afya pamoja na kuendeleza matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uuguzi na Ukunga Wizara ya Afya Bi. Ziada Sellah wakati akimkaribisha mgeni rasmi amemueleza kuwa, katika mkutano huo walipata mada mbalimbali za kujengeana uwezo ikiwemo kuwa na umuhimu wa kujituma na kufanya kazi kwa weledi.

“Kwa kweli siku hizi 3 tulipata shule ya kutosha kupitia mada mbalimbali za uongozi na utendaji kazi, ndiyo maana sasa tunaona kila mmoja ana furaha baada ya kupata maarifa mapya, tulijifunza mambo mengi ambayo yatatusaidia kuboresha utendaji wetu,” amesema Bi. Ziada