Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho, amesema Wizara hiyo imepanga kutekeleza vipaumbele vinane muhimu katika mwaka wa fedha 2026/2027 kwa lengo la kuimarisha sekta ya ulinzi, usalama na maendeleo ya taifa.
Dkt. Nyansaho amesema hayo leo Jumanne Mei 19, 2026 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Amesema miongoni mwa maeneo yatakayopewa kipaumbele ni kuimarisha Jeshi kwa zana na vifaa vya kisasa vya kijeshi, teknolojia ya mawasiliano pamoja na kuendeleza rasilimali watu ndani ya vyombo vya ulinzi.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa wanajeshi kupitia matunzo ya vifaa na zana, mafunzo, mazoezi, huduma za afya, makazi pamoja na maslahi ya askari ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo amesema Serikali imejipanga kuendelea kuimarisha uwezo wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa kuboresha miundombinu yake ili kuongeza uwezo wa kupokea vijana wengi zaidi watakaopata mafunzo ya awali ya kijeshi pamoja na stadi za kazi.
Pia, amesema Wizara itaendelea kuimarisha Jeshi la Akiba sambamba na kuendeleza na kulinda miradi ya kimkakati kwa manufaa mapana ya taifa.
Dkt. Nyansaho amesema Serikali pia inalenga kuimarisha mashirika na taasisi za utafiti wa masuala ya kijeshi pamoja na kuanzisha viwanda vipya vya sekta ya ulinzi vitakavyozalisha bidhaa kwa matumizi ya kijeshi na kiraia kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Kadhalika, amesema Wizara itaendelea kuimarisha ushirikiano na Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) katika masuala ya ulinzi na usalama.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na mamlaka za kiraia katika kukabiliana na majanga na hali za dharura pale inapohitajika.
