Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azzan Zungu, ametoa sifa za kipekee baada ya Bunge kupitisha Bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2026/2027, akieleza kuridhishwa na kazi inayofanywa na Serikali na vyombo vya ulinzi nchini.

Spika Zungu amemshukuru Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho, kwa kazi nzuri anayoifanya katika kusimamia sekta hiyo nyeti ya ulinzi na usalama wa taifa, akisisitiza kuwa utekelezaji wa majukumu ya wizara hiyo unaendelea kwa weledi na ufanisi mkubwa.

Aidha, amezipongeza pia taasisi na vyombo vya ulinzi vinavyoongozwa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jacob Mkunda, kwa kazi nzuri ya kulinda amani ya nchi na kuimarisha usalama wa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Spika Zungu amweleza kuwa Watanzania wengi mara nyingi hawajui historia ya nchi yao, akisisitiza umuhimu wa kuifahamu ili kuelewa kwa kina mchango wa Tanzania katika kulinda amani ya taifa na mataifa mengine. 

Ameongeza kuwa Tanzania imekuwa na nafasi muhimu katika kusaidia mataifa mbalimbali ambayo hapo awali yalikuwa chini ya ukoloni, kupitia juhudi za kulinda na kuendeleza amani, ambapo Jeshi la Wananchi wa Tanzania limekuwa chombo cha kuaminika katika majukumu hayo chini ya uongozi wa viongozi wakuu wa nchi kuanzia Hayati Baba wa Taifa, Julius Nyerere, hadi Rais wa sasa, Samia Suluhu Hassan.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho, ameilekeza Bunge kuwa kwa mwaka wa fedha 2026/2027 Wizara hiyo na taasisi zilizo chini yake imeomba jumla ya shilingi 4,286,489,115,000.00.

Kati ya fedha hizo, shilingi 3,859,955,462,000.00 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida, huku shilingi 426,533,653,000.00 zikitengwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo, fedha ambazo zimedhamiriwa kuimarisha shughuli za ulinzi, miundombinu na uwezo wa kiutendaji wa sekta hiyo.