Na Silivia Amandius.
Bukoba,Kagera.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kagera imeanza kutoa mafunzo kuhusu matumizi ya mfumo wa TANCIS kwa maafisa wa forodha na mawakala, ikiwa ni sehemu ya kuongeza ufanisi wa utendaji kazi katika vituo vya forodha vilivyopo mkoani humo. Mafunzo hayo pia yanatarajiwa kufanyika katika wilaya za Karagwe, Kyerwa, Missenyi na Ngara.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo leo Mei 19, 2026, Meneja Msaidizi wa Forodha Mkoa wa Kagera, Hery Talawa, amesema mafunzo hayo yatafanyika kwa muda wa siku tano yakihusisha maafisa wa TRA pamoja na mawakala wa forodha waliopo katika makao makuu ya TRA Mkoa wa Kagera.
Amesema lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwafikia watumiaji wa huduma za forodha pamoja na wananchi kwa ujumla ili kuongeza uelewa kuhusu matumizi ya mfumo huo na kuondoa changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza katika utoaji wa huduma za forodha.
Kwa upande wake, Afisa Forodha Mkuu, January Shauri, amesema mfumo wa TANCIS unatumiwa na nchi za Afrika Mashariki katika kurahisisha upatikanaji wa vibali vya forodha kwa kufuata sheria ya mwaka 2004 iliyofanyiwa maboresho mwaka 2011 pamoja na kanuni zake.
Ameeleza kuwa matumizi ya mfumo huo yamesaidia kupunguza ucheleweshaji wa huduma kutoka katika idara mbalimbali zinazohusika na shughuli za forodha, hali inayochangia kuongeza ufanisi katika biashara na usafirishaji wa mizigo.

