NA DENIS MLOWE IRINGA
KADA wa Chama Cha Mapinduzi, ambaye ni mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM Taifa ,kutokea Iringa Vijijini, Arif Abri, ameendelea na ziara yake ya kuhamasisha wananchi katika Kata ya Kising’a kujitokeza kwa wingi kumpigia kura mgombea ubunge iimbo la Isimani EmanuelaMtatifikolo wa CCM, ambapo alifanya mikutano mbalimbali katika matawi sita yaliyopo eneo hilo.
Ziara hiyo imehudhuriwa na wananchi, wazee wa kimila, viongozi wa mashina pamoja na makada wa chama wanaounga mkono juhudi za kuimarisha mwamko wa kisiasa kuelekea uchaguzi mdogo wa jimbo la Ismani.
Katika mikutano hiyo, Arif Abri aliambatana na mgombea ubunge wa Chama Cha Mapinduzi katika Jimbo la Ismani, Emanuela Mtatifikolo, ambaye alitumia fursa hiyo kujitambulisha na kueleza malengo yake endapo atapata ridhaa ya wananchi.
Katika hotuba yake, Arif Abri alisisitiza umuhimu wa wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura na kufanya maamuzi yenye kuleta tija kwa mustakabali wa Jimbo la Isimani.
Alieleza kuwa Chama Cha Mapinduzi, (CCM), kimeendelea kutekeleza miradi mbalimbali inayogusa maisha ya wananchi, ikiwemo sekta za afya, elimu, miundombinu na uchumi wa kijamii, hivyo wananchi wana kila sababu ya kuunga mkono jitihada hizo.
Ameongeza kuwa chama hicho kinaamini katika siasa za ustawi na maendeleo, na kwamba utendaji wake katika maeneo mengi nchini ni kielelezo cha dhamira ya kuwatumikia wananchi bila ubaguzi. Aliwahimiza vijana kujitokeza kwa wingi kwenye mikutano ya kampeni, kushiriki midahalo ya kisiasa kwa ustaarabu na kutoa maoni kuhusu namna ya kuboresha mustakabali wa kijamii na kiuchumi.
Kwa upande wake, Emanuela Mtatifikolo aliwashukuru wakazi wa Kata ya Kising’a kwa kujitokeza kwa wingi na kuonesha ushirikiano katika mikutano yote aliyohudhuria.
Alibainisha kuwa miongoni mwa vipaumbele vyake ni kuimarisha huduma za kijamii, kuweka mkazo kwenye fursa za kiuchumi kwa vijana na wanawake, pamoja na kusimamia uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali za umma. Alisema kwamba ushirikiano kati ya wananchi na viongozi ndicho kichocheo kikuu cha maendeleo ya kweli katika jimbo hilo.
Ziara hiyo imetajwa kuwa miongoni mwa mikutano muhimu katika kuelekea kampeni za uchaguzi, ikizingatia kwamba maeneo ya vijijini kama Kata ya Kising’a yana mchango mkubwa katika uundaji wa mwelekeo wa kisiasa wa Jimbo la Isimani. Uongozi wa Kata, pamoja na wenyeviti wa matawi ya CCM, uliipongeza hatua hiyo kama ishara ya kuendelea kuwasogelea wananchi na kusikiliza maoni yao moja kwa moja.
Kwa ujumla, mkutano huo umeonyesha mwamko mkubwa wa wananchi, huku wengi wakipongeza hatua ya viongozi hao kutembelea maeneo ya pembezoni na kuwasikiliza.
Ziara zaidi katika vijiji vingine vya Jimbo la Isimani zinatarajiwa kuendelea katika siku zijazo ikiwa ni sehemu ya mikakati ya chama kuimarisha uelewa wa wananchi kuhusu sera na mikakati yake ya maendeleo.

