Na. Ssgt Mawazo Mtondo – Dodoma.

Mkuu wa Sehemu ya Huduma kwa wafungwa (OMS)Jeshi la Magereza, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza (SACP) Emmanuel Malisa, leo Mei 17, 2026 ameongoza kikao cha wadau, marafiki na wapenzi wa timu ya Tanzania Prisons FC, ambapo amewasisitiza kuendelea kudumisha ushirikiano, umoja na mshikamano kati ya mashabiki, wachezaji, viongozi wa timu pamoja na viongozi wakuu wa Jeshi la Magereza, kwa lengo la kuimarisha maendeleo na mafanikio ya klabu hiyo.

Aidha, SACP. Malisa amesisitiza umuhimu wa mshikamano na kujitolea kwa kila mdau katika kuhakikisha timu hiyo inaendelea kufanya vizuri ndani na nje ya uwanja. Kikao hicho kimefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Jeshi la Magereza Msalato, Jijini Dodoma.

Akisoma wasilisho la rasimu ya katiba ya matawi ya marafiki wa Tanzania Prisons Sports Club, Mrakibu Mwandamizi wa Jeshi la Magereza (SSP) Bakari Sudi alisema Jeshi la Magereza lina timu inayoshiriki Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara pamoja na timu nyingine mbalimbali zinazoshiriki michezo tofauti ikiwemo riadha, mpira wa wavu, mpira wa kikapu, netiboli, mieleka, judo, magongo, vishale na ngumi.

SSP. Sudi, pia alieleza historia ya mafanikio ya Tanzania Prisons SC, akibainisha kuwa timu hiyo iliwahi kutwaa ubingwa wa Kombe la Muungano mwaka 1999, mashindano yaliyokuwa yakizikutanisha timu bora kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kwa lengo la kupata mwakilishi wa Tanzania katika michuano ya kimataifa.

Kutokana na mafanikio hayo, Tanzania Prisons SC ilipata nafasi ya kushiriki michuano ya CAF Champions League mwaka 2000 ambapo iliishia hatua ya awali. Aidha, klabu hiyo pia ilishiriki michuano ya CAF Confederation Cup mwaka 2005 na 2009, na katika misimu yote miwili iliaga mashindano hayo katika hatua za mwanzo.

Tanzania Prisons SC ni moja ya klabu zinazojivunia kuwa na mashabiki wengi nchini, ambapo wengi huamini kuwa baada ya klabu za Simba SC na Yanga SC, Tanzania Prisons SC ni miongoni mwa timu inayofuatia kwa kuwa na wapenzi na mashabiki wengi wa soka hapa nchini.

Kwa sasa Tanzania Prisons SC ipo katika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 17 baada ya kucheza michezo 23, huku ikiendelea kupambana kujinasua kutoka maeneo ya chini ya msimamo na kusaka matokeo bora katika michezo iliyosalia ya msimu huu.