NA: MWANDISHI WETU, PANGANI
Timu kutoka Kata ya Bweni ya wilaya ya Pangani imefanikiwa kuibuka mshindi wa mashindano ya Aweso Vijana Cup kwa ushindi wa magoli (5-4) dhidi ya timu ya Kimang’a, ushindi uliopatikana kwa njia ya penati.
Mechi ya fainali hiyo imechezwa Mei 16, 2026, katika uwanja wa Kumba ambapo timu ya Bweni na Kimang’a zilitoka sare ya goli (1-1) katika dakika 90 za mchezo.
Baada ya hapo, timu hizo ziliingia katika kupiga penati, ambapo timu ya Bweni ilipata penati zote tano huku timu ya Bweni ikipata penati nne na kukosa penati moja, jambo lililoipata ubingwa timu ya Bweni.
Katika fainali hiyo, Mbunge wa Pangani na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ambaye alikuwa Mgeni Rasmi, alizipongeza timu zote zilizoshiriki mashindano hayo, na ameahidi kuendelea kufadhili michezo ili wilaya ya Pangani ing’are kimichezo.
“Kwa kuwa mimi ni mdau wa michezo, naahidi kutoa laki tano, jezi seti moja na mpira mmoja kwa timu zote zilizoshiriki mashindano haya. Vilevile, katika mashindano yajayo nitatoa zawadi nono ya shilingi milioni kumi kwa mshindi wa kwanza na milioni tano kwa mshindi wa pili, siitaki zawadi za mbuzi kwa vijana wangu,” amesema Aweso.
Katika hatua nyingine, Aweso amewahimiza wanawake kuanzisha mashindano yao na yupo tayari kuyadhamini na bingwa ataibuka na kitita cha millioni kumi na mshindi wa pili atapata milioni tano.
Katika kuchochea michezo mashuleni, Aweso amesema atatoa vifaa vya michezo kwa shule zote za msingi na sekondari za serikali na binafsi ili kuibua na kuendeleza vipaji vya wanafunzi.
Mratibu wa mashindano hayo, Ramadhani Kibendera amesema mashindano hayo yameibua vipaji vya vijana na wakiwezeshwa watafika mbali.
Awali, kabla ya kuchezwa kwa mchezo wa fainali, kulitanguliwa michezo kadhaa wa kadha kama kukimbia mbio (jogging), rede, mpira wa wavu, pete, bonanza la bodaboda na mashabiki wa Simba na Yanga ambapo lengo ni kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi, kukuza vipaji vya vijana ikiwa ni njia ya kujipatia kipato kupitia michezo.

