NA DENIS MLOWE IRINGA

MBUNGE wa Jimbo la Kalenga, Jackson Kiswaga, ametoa pongezi kwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji mkubwa wa miradi ya maendeleo katika jimbo hilo, huku akiwasilisha changamoto zinazohitaji ufumbuzi wa haraka ikiwemo upatikanaji wa maji, mabweni ya wanafunzi na vituo vya afya.

Akizungumza mbele ya Waziri Mkuu wakati wa mkutano wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi uliofanyika katika viwanja vya Ifunda Sokoni, Kiswaga alisema wananchi wa Kalenga wameendelea kunufaika na uwekezaji mkubwa wa serikali katika sekta mbalimbali za maendeleo.

KIswaga alimshukuru Waziri Mkuu kwa ziara zake za mara kwa mara zinazolenga kusikiliza changamoto za wananchi moja kwa moja na kuzitafutia ufumbuzi.

Alikumbusha kuwa eneo la Ifunda lina historia ya kutembelewa na viongozi wakuu wa serikali, akitaja ziara ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, mwaka 2021 ambapo alichangia kutatua changamoto mbalimbali za maendeleo.

Kiswaga alisema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Jimbo la Kalenga limepokea zaidi ya shilingi bilioni 19.2 kupitia fedha za maendeleo ambazo zimewezesha ujenzi wa shule mpya za sekondari nne, shule za msingi mbili, vituo vya afya vitatu, vyumba vya madarasa 146, mabweni 17 na maabara tisa za sayansi.

Aidha, alisema sekta ya afya imeimarishwa kupitia ukamilishaji wa zahanati nne na miradi mbalimbali ya kuboresha huduma za afya, huku serikali ikitoa zaidi ya shilingi bilioni 3.8 kwa ajili ya kukamilisha jengo la utawala pamoja na nyumba za viongozi wa halmashauri.

Katika sekta ya kilimo, Kiswaga alisema wakulima wa Kalenga wameendelea kunufaika na mbolea ya ruzuku, huku serikali ikijenga majosho matatu ya mifugo na kuendelea kutoa mikopo kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.

Mbunge huyo pia alieleza mafanikio yaliyopatikana katika upatikanaji wa umeme vijijini na ujenzi wa barabara mpya nne zilizofungua mawasiliano katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo.

Pamoja na mafanikio hayo, Kiswaga alisema changamoto kubwa inayolikabili jimbo hilo ni upatikanaji wa maji safi na salama kutokana na ukosefu wa vyanzo vya uhakika.

Alieleza kuwa miradi kadhaa ya maji inaendelea kutekelezwa katika maeneo ya Ifunda, Ikungwe, Kalenga na Ulelu Kibebe huku mingine ikiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Alisema hivi karibuni serikali imetoa shilingi milioni 630 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kihanga, pamoja na shilingi milioni 583.8 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya sekondari na shilingi milioni 160 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni katika shule za sekondari za Lupembelwasenga na Rumuli.

Kiswaga alisisitiza kuwa licha ya Kalenga kuwa na shule za sekondari katika kila kata, bado kuna upungufu mkubwa wa mabweni unaosababisha wanafunzi kutembea umbali mrefu na kuongeza hatari ya changamoto mbalimbali za kijamii.

Alitoa wito kwa serikali kuendelea kujenga mabweni katika shule zote za sekondari za kata ili kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi, hususan wanaotoka maeneo ya mbali.

Katika hatua nyingine, Mbunge huyo alieleza kuwepo kwa migogoro ya ardhi katika kata za Wasa, Lumuli na Maboga, akitaka uwekezaji wowote wa ardhi kufanyika kwa kushirikisha wananchi na serikali za vijiji ili kuepusha migongano isiyo ya lazima.

Kiswaga alisema changamoto kuu zinazohitaji msukumo zaidi wa serikali ni upatikanaji wa maji, maboresho ya miundombinu ya barabara, kuimarisha huduma za umeme, ukarabati wa shule kongwe za msingi pamoja na kuongeza idadi ya walimu na vituo vya  afya katika kata.