Serikali imejipanga kuondosha adha ya huduma ya maji kwa wakazi wa Chemba.

Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali itahakikisha Mradi wa Maji wa Miji 28 katika Mji wa Chemba unakamilika kwa wakati na kuondoa uhaba wa huduma ya majisafi na salama kwa wananchi.“Chemba imekuwa ikikumbwa na changamoto ya ukame na uhaba wa maji, hivyo Serikali imejipanga kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji ya uhakika,” Dkt. Nchemba amesema akiwa katika ziara wilayani hapo.

Amekagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa Maji wa Miji 28 Chemba unaotekelezwa na Wizara ya Maji.

Mkurugenzi wa Usambazaji Maji wa Wizara ya Maji Mhandisi Charles Mafie amesema mradi huo unathamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 11 na utekelezaji umefika asilimia 76, ukitarajiwa kuhudumia zaidi ya wananchi elfu 18 wa Mji wa Chemba pamoja na vijiji vya Chemba, Chambalo, Kambi ya Nyasa, Gwandi, Paranga na Makamaka.

Mradi unahusisha ujenzi wa visima vitatu vyenye uwezo wa kuzalisha lita za maji 207,000 kwa saa, ujenzi wa matenki ya kuhifadhi maji, kituo cha kusukuma maji pamoja na ulazaji wa mabomba ya usambazaji yenye urefu wa kilomita 60.Baada ya kukamilika, mradi huo unatarajiwa kuongeza hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kutoka asilimia 37 ya sasa hadi asilimia 100, ambapo uzalishaji wa maji utaongezeka kutoka wastani wa lita 170, 000 kwa siku hadi zaidi ya lita 3,000,000 ambayo ni hatua kubwa itakayobadilisha maisha ya wananchi wa na kuongeza kasi ya maendeleo katika uchumi na jamii